IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Jeshi la Iran liimarishwe ili adui asiwaze kuishambulia nchi

4:59 - October 02, 2015
Habari ID: 3377230
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa vikosi vya jeshi la Iran vinapaswa kuzidisha kasi ya maendeleo na kuzidisha utayarifu wake kwa kadiri kwamba, adui asithubutu hata kuwa na fikra ya kuihujumu Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil  Udhma Sayyid Ali Khamenei aliyasema hayo Akhamisi alipohutubia  hadhara ya makamanda wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu kaskazini mwa nchi. Aliongeza kuwa, sababu ya uadui unaofanywa dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ni kusimama kidete kwa taifa la Iran, uwazi na kutosalimu amri kwake mbele ya siasa za ubeberu. Amesisitiza kuwa vikosi vya jeshi la Iran vinapaswa kuzidisha kasi ya maendeleo na kuzidisha utayarifu wake kwa kadiri kwamba, adui asithubutu hata kuwa na fikra ya kuihujumu Iran.
Ayatullah Khamenei amesema, ni jambo la dharura kuweka mikakati ya mustakbali bora na wenye maendeleo makubwa zaidi wa Iran ya Kiislamu katika nyanja zote. Amesema kuwa mustakbali wa Iran uko mikononi mwa vijana na kwa msingi huo kuna udharura wa kujua thamani yao. Ameongeza kuwa, kuna ulazima wa kulea kizazi kilicho tayari zaidi, chenye azma kubwa zaidi, chenye elimu na ujuzi mkubwa zaidi na shujaa zaidi ili Iran ya kesho iweze kudhihiri na uwezo na nguvu kubwa zaidi na kuwa na ushawishi katika eneo la Mashariki ya kati na ulimwenguni.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kubakia nyuma kihistoria hapa nchini kutokana na tawala za watu tegemezi hususan katika kipindi cha utawala wa Kipahlavi na akasema: Maendeleo ya sasa ya vikosi vya jeshi katika nyanja mbalimbali yana thamani kubwa lakini kwa kutilia maanani kubakia nyuma huko, kuna ulazima wa kuzidisha kasi ya harakati na kuimarisha nguvu ya jeshi kiasi kwamba maadui wasithubutu hata kuwa na fikra ya kushambulia mipaka ya nchi hii.
Amesema mapambano na kusimama kidete kwa taifa la Iran katika kipindi cha miaka 8 ya kujihami kutakatifu ni tajiriba na uzoefu muhimu mbele ya dunia nzima na kuongeza kuwa: Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni mfumo unaojitawala na tangu mwanzoni mwa Mapinduzi umekuwa ukiendeleza siasa zake kwa uwazi na hautishwi na dola lolote lile au kuogopa kupinga siasa za dola hilo. 
Ayatullah Khamenei amegusia pia uadui mkubwa na mzito uliopo dhidi ya harakati huru na ya kustaajabisha ya taifa la Iran na kusema: Adui anataka kuufanya mfumo wa Kiislamu usalimu amri; na kulegeza misimamo mbele ya adui hakuwezi kukomesha uadui.
Kiongozi Muadhamu amesema, mfumo wa kibeberu unashindwa kustahamili suala la kujitokeza taifa huru linalopinga madhalimu na vibaraka wao, kwa msingi huo unafanya uhasama na uadui dhidi ya taifa hili; na kunadhani kwamba kama hatutasema neno fulani au kama hatutafanya jambo fulani suala hilo litapunguza uadui, ni dhana isiyo sahihi.
Ameashiria mapokezi na uungaji mkono mkubwa wa mataifa mbalimbali na vilevile baadhi ya serikali zisizo tegemezi kwa harakati huru ya Iran na kusema: Mataifa mbalimbali yanafurahishwa mno na maendeleo na jinsi taifa Iran inavyotetea waziwazi maslahi yake mbele ya madola makubwa, na katika safari za nje za maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia wakati wote serikali zinapowaruhusu wananchi kuonesha mapenzi yao (kwa Iran) wamekuwa wakionesha mapenzi yao makubwa.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amezungumzia umuhimu wa kufanya utafiti na maendeleo ya uhakiki katika Jeshi la Taifa na kusema: Kuna uwanja nzuri sana katika vyuo vikuu na vituo vya utafiti hapa nchini na lazima uhusiano wa kielimu wa vikosi vya jeshi na vituo hivyo uimarishwe zaidi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza umuhimu wa kuingia katika nyanja ambazo hazijatambulika za kijeshi na uvumbuzi mpya hususan katika mazoezi ya kijeshi na kusema: Mazoezi ya kijeshi yanapaswa kukaribia anga ya vita na uhakika wa medani za vita na kuwepo utayarifu na tathmini ya zana na uwezo wote wa adui.
Mwanzoni mwa mkutano huo Admeri Sayyari ambaye ni kamanda wa Jeshi la Majini la Iran ametoa ripoti kuhusu majukumu na shughuli za jeshi hilo katika nyanja za utengenezaji wa zana, masuala ya mawasiliano, operesheni za kijeshi, ustawi wa kielimu, teknolojia ya mawasiliano na kadhalika.

3377059

captcha