IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Mabeberu wamepanga vita laini dhidi ya Mfumo wa Kiislamu Iran

21:15 - October 12, 2015
Habari ID: 3384712
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) ni ngome hai na ya mstari wa mbele ya kukabiliana na vita laini.

Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo mbele ya hadhara ya Mkuu pamoja na Wakurugenzi wa Shirika la Utangazaji la Redio na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Akibainisha malengo ya "vita laini vikubwa na vilivyoratibiwa vya mfumo wa ubeberu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran", Ayatullah Khamenei amesema kuzibadilisha imani na itikadi za wananchi ndilo lengo kuu zaidi la vita hivyo tata; hivyo amesisitiza juu ya nafasi ya kipekee ya IRIB katika vita hivyo vikali. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria umuhimu wa Shirika la Utangazaji katika Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na jinsi linavyolazimika bila kutaka kukabiliana na vitatizi na hatari za vita laini na akaongezea kwa kusema: vita laini, kinyume na vita vigumu havihisiki, havifahamiki na wala haviko wazi, bali hata kuna wakati hutoa pigo huku jamii inayolengwa ikiwa kwenye maruerue ya usingizi na kushindwa kulihisi shambulio hilo. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kujenga ndani ya fikra za vijana imani zisizowiyana na uhalisia halisi kuhusu ulimwengu hususan wa Marekani na Ulaya kwa kuzionesha kuwa ni nchi zilizoendelea, zenye raha, amani na zisizo na matatizo yoyote, ni miongoni mwa malengo mengine ya vita laini, na akafafanua kwamba: ghaya na lengo kuu la vita laini vilivyoratibiwa ni kuleta mmomonyoko wa ndani kwa ndani katika Jamhuri ya Kiislamu kupitia ugeuzaji itikadi na udhoofishaji imani za wananchi hususan vijana. Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa katika kufanikisha malengo ya vita laini, kwa adui si muhimu kubakia jina la "Jamhuri ya Kiislamu" au hata kuwepo katika uongozi wake wa juu kabisa mtu mwenye kilemba; muhimu ni kuona Iran inadhamini malengo ya Marekani, Uzayuni na mtandao wa madola yenye nguvu duniani. Ayatullah Khamenei aidha amekumbusha kuwa Shirika la Utangazaji ni chombo cha habari cha Mfumo na Mapinduzi ya Kiislamu; na wakuu na wafanyakazi wake ni majemadari na askari wa vita laini.

3384481

captcha