Hiyo ni kauli ya Professor Abdulaziz Sachedina, profesa na Mwenyekiti wa Kitivo cha Masomo ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha George Mason huko Fairfax, Virginia nchini Marekani. Profesha Sachedina yuko Tehran kuhudhuria kongamano la kimataifa la "Qur’ani Katika Sirah na Fikra za Imam Khomeini MA".
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano ya IQNA na Profesa Sachedina.
Suali: Kwanza tufafanulie kuhusu makala yake katika kongamano hili?
Jibu: Nimealikwa kuwasilisha makala kuhusu uhusiano baina ya kiongozi Imam Khomeini na Qur'ani Tukufu. Kwa maoni yangu, kongamano hili ni muhimu sana kwani katika kipindi hiki tunapaswa kurejea katika mafundisho ya Qur'ani Tukufu na Imam Khomeini ambaye alifanikisha mapinduzi kwa malengo yake mazuri kwa watu wa Iran na Waislamu kote duniani. Qur'ani ilikuwa chanzo cha ilhamu kwa Imam Khomeini na kwa njia hiyo aliweza kuzungumza na dunia na Waislamu kote duniani.
Naweza kusema kuwa, kila ambaye anatafakari kuhusu msingi wa kimaanawi wa uwepo wa mwanadamu na ujumbe wa Qur'ani kuhusu umaanawi katika zama zetu hizi, anapaswa kusoma aliyoyasema Imam Khomeini MA kuhusu Qur'ani Tukufu.
Suali: Umeashiria ujumbe wa kimataifa. Sisi tunaishi katika karne ya 21 na Waislamu wanakumbwa na changamoto na migogoro. Unaweza kufafanua zaidi kuhusu kauli yako hiyo kwa kuzingatia hali ya hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu.
Jibu: Swala muhimu linaloikabili dunia na Waislamu kote duniani ni kuweka wazi kile tunachoita kuwa ni, "hali na dhati ya haki na batili." Tuko katika mikakati ya ustawi wa kiuchumi, maendeleo ya kisiasa na nukta nyinginezo za uwepo wa mwanadamu kijamii kote duniani. Kwa hivyo, zaidi ya wakati wowote ule, hivi sasa tunadiriki maana ya muelekeo wa kimataifa wa Qur'ani Tukufu kama alivyobainisha Imam Khomeini MA. Hivi sasa tunatafuta mlingano. Kwani tunakabiliwa na misimamo ya kufurutu ada ya kimada na misimamo mikali na ya kimabavu ya kundi kama ISIS au Daesh n.k. Kwa hivyo unaweza kutasawari kuwa kuna mtu moja ambaye anaweza kuathiri mtu binafsi, jamii, taifa na jamii ya kimataifa. Unaweza kuanza na mtu binafsi na kisha kuunda taifa kama alilounda Imam. Nimemjua Imam Khomeini kwa muda mrefu. Nina umri wa miaka 73 na nimeishi katika maeneo mengi ya dunia. Hivi sasa ninadiriki yale ambayo Imam Khomeini alitufunza miaka 40 iliyopita. Alitupa mafunzo ya kimataifa. Hivi sasa wengi tunataka kuwa matajiri na wenye mafanikio. Haya ni mambo ambayo yanatupelekea kuchunguza aina mbali mbali za fikra na idiolojia. Kile kilicho muhimu ni kuwa mwanadamu. Iwapo sehemu moja ya jamii ya mwanadamu inauma basi wanaadamu wote wahisi uchungu. Kwa mujibu wa Imam Khomeini, iwapo utapuuza masaibu ya wengine hilo linamaanisha kuwa hujali majukumu yako ya kimaadili.
Kwa Imam Khomeini, Qur'ani ilikuwa chimbuko la ilhamu na hapa tunaweza kuashiria Aya ya 70 ya Sura Al-Israa: "Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba."
Mwenyezi Mungu amewatukuza na kuwaheshimu wanaadamu wote pasina kujali jinsia, rangu, ukabila, n.k. Huu ulikuwa moyo wa Qur'ani ambao tunaupata katika ujumbe wa Imam Khomeini.
Abdulaziz Sachedina ni profesa na Mwenyekiti wa Kitivo cha Masomo ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha George Mason huko Fairfax, Virginia nchini Marekani. Amekuwa profesa kwa muda wa miaka 33. Alizaliwa nchini Tanzania na alipata shahada zake za Uzamili (MA) na Uzamivu (PHD) kutoka Chuo Kikuu cha Toronto. Alipata shahada za kwanza za BA kutoka Chuo Kikuu cha Waislamu cha Aligarh, India na Chuo Kikuu cha Ferdowsi, Masshad, Iran. Alikuwa kati ya wanafunzi wa hayati Dr. Ali Shariati nchini Iran. Anazungumza lugha za Kihindi, Kiurdu, Kifarsi, Kiarabu, Kigujarati, Kiswahili, Kiingereza, Kiturki na Kijerumani.