Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyed Hassan Nasrallah amesema utawala haramu wa Israel unahofia mwamko au Intifadha ya Wapalestina. Sayyed Nasrallah ametoa tamko hilo Ijumaa wakati akilihutubai taifa la Lebanon kuhusu namna Israel inavyokalia kwa mabavu ardhi za Palestina sambamba na kuwakadamiza Wapalestina. Kiongozi wa Hizbullah amesema Israel iko katika mstari wa mbele wa ubeberu na uistikbari wa kimataifa.
Sayyed Nasrallah amesema watu wa Palestina wanaongoza katika mapambano na muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Amesema kile kinachojiri hivi sasa Palestina ni ishara ya imani thabiti ya Wapalestina katika mapambano yao dhidi ya Wazayuni maghasibu.
Akiendelea na hotuba yake, Sayyid Nasrallah amezikosoa baadhi ya nchi za Kiarabu kwa kutounga mkono mapambano ya kupigania ukombozi wa Palesitna. Amesema ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya nchi za Kiarabu zikiunga mkono wanamgambo huko Syria na Afghansitan lakini zinapuuza kuwaunga mkono Wapalestina. Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema utawala wa Kizayuni wa Israel ni hatari kwa usalama wa Mashariki ya Kati. Sayyid Nasrallah amesema harakati za mapambano huko Lebanon na Palestina ni chanzo cha kufeli na kusambaratike ile ndoto waliokuwa nayo Wazayuni ya, 'Israel Kubwa'. Kiongozi wa Hizbullah pia amesisitiza kuwa kadhia ya ukombozi wa Palestina haiwahusu Wapalestina tu bali ni kadhia ya ulimwengu mzima wa Kiislamu.