Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo mbele ya hadhara ya wakuu wa vyuo vikuu, vituo na taasisi za elimu ya juu, vijiji vya sayansi na teknolojia na vituo vya utafiti vya Iran, ambapo ameashiria nafasi ya elimu ikiwa ni wenzo wa nguvu na maendeleo na kuongeza kuwa vyuo vikuu ni kituo muhimu zaidi cha kuandaa viongozi wa baadaye wa nchi. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia mipango inayoandaliwa na Wamagharibi kwa ajili ya nchi wanazoziita za ulimwengu wa tatu kwa madhumuni ya kuandaa viongozi kulingana na fikra na mtindo wa maisha wa Kimagharibi kupitia vyuo vikuu na akaongezea kwa kusema, katika kutekeleza mpango wao huo nchini Iran wamekabiliwa na matatizo kutokana na utambulisho wa Kiirani na vilevile kwa sababu ya kuenea na kukita fikra za Kiislamu na za kidini miongoni mwa wanachuo na watu wa vyuo vikuu. Ayatullah Khamenei ameutaja "Ukoloni" na "bomu la atomiki" kuwa ni mifano miwili ya kihistoria ya matokeo ya kuitumia elimu katika njia isiyo sahihi na kuongeza kuwa: inapasa kujichunga muda wote kwa kuhakikisha akhlaqi na umaanawi vinaambatana pamoja na elimu. Ayatullah Khamenei ameashiria suala la uzalishaji urani kwa kiwango cha asilimia 20 uliofanywa na wanasayansi vijana wa Kiirani na kueleza kwamba: katika kipindi fulani, fueli ya tanurinyuklia la Tehran linalozalisha dawa za miale ilikuwa inakaribia kumalizika, na Wamagharibi wakatoa masharti ya udhalilishaji kwa ajili ya kutoa fueli hiyo, lakini vijana hodari na waumini wa Iran walifanya jitihada kutwa kucha na kuweza kuzalisha urani ya kiwango cha ubora wa asilimia 20 na kukidhi mahitaji ya nchi. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha pia kwamba: leo hii vyuo vikuu na wanachuo wanaandamwa na dhoruba za njama kubwa kabisa; na maadui wa nchi wana kiwewe kutokana na kuwepo katika medani za elimu wanaakademia wa vyuo vikuu wenye moyo wa kimapinduzi, kwa kuvuka mistari yao myekundu waliyoweka, kwa kupeperusha bendera ya elimu na kwa kuzinawirisha sha'ar za kimapinduzi; na kwa sababu hiyo maadui hao wanapanga mipango na kutumia gharama kubwa ili kukabiliana na harakati hiyo.