Ayatullah Udhma Sayyid
Ali Khanei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo leo
asubuhi aliponana na maelfu ya wajumbe wa Umoja wa Jumuiya za Kiislamu za
Wanafunzi kutoka kona zote za Iran na kusema kuwa, moja ya medani muhimu za
mapambano baina ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kambi ya kiistikbari na
kibeberu ni suala la vijana. Amesisisitiza kuwa: Kambi inayopambana na mfumo wa
Jamhuri ya Kiislamu inapigania kubadilisha utambiulisho wa kidini na kimapinduzi
wa vijana wa Iran na kuwakoponya matumaini, nishati na mori wao, na kwamba njia
pekee ya kukabiliana na mashambulio hayo ya siri na tata, ni kulea vijana
walioshikamana na dini, wanamapinduzi, wema, wenye misimamo thabiti, wenye
mwamko, wenye matumaini na hamasa kubwa, mashujaa na walio tayari kujitolea
wakati wote katika njia ya haki na kuwafanya vijana hao kuwa maafisa wa vita
laini.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewausia
vijana nchini kutumia vizuri sana fursa hii yenye thamani kubwa ya mwezi wa
Rajab na baadae Shaaban na Ramadhani na kusema kuwa: Kipindi cha miezi hii
mitatu ni kipindi bora kabisa cha kujijenga kimaanawi na kwamba vijana ambao
wako katika kipindi bora na muhimu mno cha umri wao wanaweza kustafidi vizuri
sana na fursa hii yenye thamani kubwa kwa ajili ya kujiimarisha kimaanawi.
Baada ya hapo, Ayatullah Udhma Khamenei ametaja baadhi ya medani za mapambano
baina ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kambi ya kiistikbari inayoongozwa na
Marekani na Uzayuni na kusema kuwa: Uhuru wa nchi ni pamoja na uhuru wa
kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni na hiyo ni moja ya medani hizo za mapambano
kwani madola ya kibeberu yanakabiliana na nchi yoyote ile inayoamua kusimama
kidete kupambana na uistikbari wa mabeberu hao na kulinda uhuru wake.
Aidha amelitaja suala la maendeleo ya nchi kuwa ni medani nyingine ya mapambano
baina ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kambi ya kiistikbari na kusema kuwa:
Madola ya kibeberu duniani yanakabiliana na kila nchi ambayo imeamua kujiletea
maendeleo yake bila ya kuyategemea madola hayo kwani madola hayo yanatambua
vyema kuwa, maendeleo ya namna hiyo huwa funzo na kigezo kizuri kwa mataifa
mengine duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema kuwa, hiyo ndiyo
moja ya sababu kuu ya madola ya kiistikbari kusimama na kukabiliana na Iran na
kujaribu kulizuia taifa hili kumiliki teknolojia ya nyuklia na kusisitiza kuwa:
Kama tutalegeza kamba katika kukabiliana na madola hayo, basi bila ya shaka
yoyote upinzani wa madola hayo kwa maendeleo yetu katika nyuga nyingine za
bioteknolojia, teknlojia ya Nano pamoja na nyuga nyinginezo za maendeleo
utakuwa mkubwa zaidi kwani madola hayo yanapinga maendeleo yoyote yale ya
kielimu, kiuchumi na kiustaarabu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja nafasi muhimu sana ya Iran katika eneo la
magharibi mwa Asia na kushiriki kwake vilivyo katika masuala muhimu duniani,
kadhia ya Palestina, suala la muqawama na kadhia ya mtindo wa maisha wa
Kiirani-Kiislamu kuwa ni uwanja mwingine wa mapambano baina ya Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran na kambi ya kiistikbari. Amesisitiza kuwa: Kama mtindo wa
maisha wa Kimagharibi utaeneo katika nchi fulani, basi itakuwa ni jambo rahisi
kupenya katikati ya watu muhimu na wenye vipawa wa jamii ya nchi hiyo na
kuwazuia kukabiliana na siasa za kibeberu.
Vile vile amezungumzia suala la vijana ambao ni moja ya medani muhimu sana za
mapambano baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kambi ya kiistikbari na
kusema kuwa: Hivi sasa kuna vita vikubwa laini vya chini kwa chini baina ya
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa upande mmoja na Marekani na Wazayuni kwa upande
wa pili kuhusiana na suala la vijana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, vijana wanafunzi wa shule
za msingi, sekondari na vyuo ndio maafisa wa vita hivyo laini na kuongeza kuwa:
Katika vita hivi laini tunaweza kusema kuwa kuna maafisa wa aina mbili wenye
utambulisho tofauti na matokeo ya vita hivyo nayo yanaweza kuwa tofauti
kulinganana na aina ya maafisa wenyewe.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, vita laini ni hatari zaidi kuliko vita
vya kutumia silaha za kijeshi na kuashiria baadhi ya upayukaji wa maadui na
kusema kuwa: Baadhi ya wakati wanatutishia vita vya moja kwa moja vya silaha
jambo ambalo ughalati wake umepindukia mipaka kwani hawathubutu hata kidogo
kufanya jambo kama hilo na hata tujaalie itokezee wafanye ghalati kama hiyo,
basi watakula kipigo wasichokitarajia.
Ameashiria pia namna vita laini dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
vinavyoendelea hivi sasa na ulazima wa taifa la Iran kufikiria pia kushambulia
badala ya kujihami tu, na kusisitiza kwamba: Kama katika kambi na ngome ya
kivita kutakuwa kuna maafisa walioshikamana vilivyo na dini, wanamapinduzi,
wenye misimamo isiyotetereka, wenye mwamko, wachapakazi, wanafikra, mashujaa na
walio tayari kujitolea muhanga katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi inawezekana
kutabiri mapema matokeo ya pambano hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Lakini kama katika
kambi na ngome ya vita hivi laini kutakuwa na maafisa walio tayari kusalimu
amri, kudanganya na wanaopumbazwa na vicheko na tabasamu za adui, maafisa wasio
na mori wala fikra, wasiojali mustakbali wao na wala wa wenzao na wakawa
wanashughulishwa tu na starehe na hawaa za nafsi, basi bila ya shaka yoyote
matokeo ya vita hivyo nayo yanajulikana.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kwa kkuzingatia yote hayo tutaona
kuwa, katika vita laini inawezekana kukawa na maafisa wa aina mbili wenye
utambulisho na hali tofauti, aina moja ni ya maafisa wanaokubaliwa na Jamhuri
ya Kiislamu na aina ya pili ni ya maafisa wanaokubaliwa na kambi ya kiistikbari
na aina zote mbili za maafisa hao zinaweza kubadilisha kabisa hatima ya vita
hivyo.
Vile vile amesrma kuwa, inaposisitiziwa wajibu wa vijana kushikamana na dini na
kuwa wasafi na wacha Mungu na kujiweka mbali na pumbao la kidunia na hawaa za
nafsi hakuna maana kabisa ya kufungamanishwa suala hilo na taasubu, fikra
mgando na kutoona mbali. Amesema: Wamagharibi na hasa Wamarekkani wanafuatilia
kwa karibu kuona vijana wa Iran wanageuka na kuwa watu wasio na imani, wasio
mashujaa, wasio na mori na msukumo wowote, wasio na harakati, wasio na
matumaini na vile vile wanaowaangalia kwa jicho zuri maadui na wenye mtazamo
mbaya na dira na mustakbali wao. Lakini mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unapigania
kujenga na kulea vijana tofauti kabisa na matarajio na ndoto hizo za kambi ya
kiistikbari.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amezitaka kwa kugogoteza
jumuiya za Kiislamu za wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo kutilia
mkazo suala la kulea vijana wenye muundo na utambulisho wa kidini na kueneza
moyo huo kwa vijana wenzao wote wa rika lao na kuongeza kuwa: Kama ambavyo tuna
mipango ya muda mrefu ya harakati ya kielimu, kidini na kimapinduzi kwa ajili
ya vijana wetu nchini, adui naye ana mipango ya muda mrefu ya kukabiliana na
mipango yetu hiyo na kwamba njia pekee ya kukabiliana na kambi hiyo ya maadui
ni kuongeza kiwango cha ubora na idadi ya vijana wanamapinduzi nchini
walioshikamana vilivyo na dini na wasioyumba wala kutetereka hata kidogo.
Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia majukumu
ya viongozi nchini Iran kuhusu vijana huku akisisitiza kwamba Wizara ya Elimu
na Malezi nchini ina watu walioshikamana na dini na inabidi fursa hiyo muhimu,
itumike vizuri sana. Amesema, mbali na shule kutoa mafunzo ya kielimu na ya
kufundisha madarasani, zinapaswa kuwa na ratiba nyingine sahihi za
kuwashirikisha wanafunzi katika kazi za kimapinduzi ili kuhakikisha kuwa kizazi
cha vijana kinakuwa ni kizazi cha wanamapinduzi.
Vile vile ameisihi Wizara ya Elimu na Malezi nchini kutoa mwanya na fursa kwa
vyama na jumuiya za kimapinduzi kama vile Umoja wa Jumuiya za Kiislamu za
Wanafunzi na Basiji ya Wanafunzi na kuongeza kuwa: Kuna habari kwamba baadhi ya
shule zinapinga kufanyika kazi za kimapinduzi katika shule hizo, hivyo Wizara
ya Elimu na Malezi inapaswa kukabiliana vizuri na jambo hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema pia kuwa, mazingira ya Iran
ya kuwa na vijana wengi ni mazingira yanayotia matumaini na kusisitiza kuwa:
Pamoja na kuwepo smambo mbali mbali ya upotoshaji na licha ya kuwepo kambi
kubwa ya maadui lakini bado nchini Iran kuna vijana waumini, wanamapinduzi,
watu wa tawassul, watu wa kutembea masafa marefu kwa miguu wakati wa Arubaini
(ya Imam Husain AS), watu wa Qur'ani, watu wa itikafu, watu wenye misimamo
imara na watu wanaosimama kidete katika medani za kuyalinda Mapinduzi ya
Kiislamu, na inabidi tumshukuru sana Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa neema hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, kuwepo vijana hao
nchini Iran ni jambo adhimu sana na kusisitiza kuwa, baada ya kupita miaka 37
ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kambi ya kiistikbari hadi sasa imeshindwa
kuiondoa katika uso wa dunia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran au kuizuia kustawi na
kupata nguvu katika eneo hili na kuongeza kuwa: Pamoja na kuwepo vitisho
vikubwa vya kivitendo na kipropaganda vya maadui lakini leo hii Hizbullah ya
Lebanon imethibitisha kupevuka kwake katika ulimwengu wa Kiislamu na kwamba
kitendo cha serikali fulani fasidi, kibaraka, pumba na isiyo na chochote ndani
cha kuilaani harakati hiyo katika kipande fulani cha karatasi; hakina umuhimu
wowote ule.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia namna utawala wa Kizayuni wa Israel
ulivyokula kipigo kutoka kwa Hizbullah katika vita vya siku 33 na kulinganisha
na jinsi jeshi la nchi tatu zenye nguvu za Kiarabu zilivyoshindwa vitani na
utawala wa Kizayuni na kusisitiza kuwa: Hizbullah na vijana wake walioshikamana
vilivyo na dini wanang'ara mithili ya jua na ni fakhari kwa ulimwengu mzima wa
Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema, dhati ya harakati
zinazopigania haki duniani inazidi kuimarikana na kuongeza kuwa: Kuna uwezekano
haki ikakumbwa na misukosuko mingi lakini hatima ya yote, haki ndiyo
inayoshinda.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, sharti kuu la kuweza kushinda haki ni
kusimama imara maafisa wa vita laini katika kukabiliana na matatizo mbali mbali
na kusisitiza kuwa: Haki ni ya vijana (wa Iran ambao ni maafisa wa vita laini)
na kwa taufiki na uwezo wa Mwenyezi Mungu, kuna siku matatizo yote yataondoka
pole pole na vijana wetu watafikia kwenye vilele vya juu vya mafanikio.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam
Walmuslimin Hajj Ali Akbari, mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu katika Umoja wa
Jumuiya za Kiislamu za Wanafunzi ametoa ripoti fupi kuhusu kazi za taasisi hiyo
na kusema kuwa: Malengo na shabaha zetu kuu leo hii ni kulea wanafunzi wenye
hadhi na daraja inayotakiwa na Mapinduzi ya Kiislamu na ni kwa sababu hiyo ndio
maana malezi ya Kimapinduzi kwa kutumia mafundisho ya Kialawi, yakawa ndiyo
ajenda kuu ya ratiba na mipango yetu yote.
Vile vile wanafunzi wawili wanachama wa Umoja wa Jumuiya za Kiislamu za
Wanafunzi wamepata fursa ya kuzungumza mbele ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi
ya Kiislamu na kutoa mitazamo, madukuduku na daghadagha zao kuhusu kazi na
harakati za wanafunzi na masuala ya vijana, masomo na malezi mashuleni.