IQNA

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran

Waislamu wawe na umoja ili wakabiliene na maadui wa Uislamu

22:21 - June 17, 2016
Habari ID: 3470392
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran ametoa wito kwa mataifa yote ya Waislamu kuwa na umoja mbele ya njama za ustikbari na Uzayuni wa kimataifa dhidi ya Dini Tukufu ya Uislamu.

Ayatullah Muhammad Imami Kashani amesema katika hotuba ya Swala ya Ijumaa hapa Tehran kuwa leo hii sura ya uistikbari na Uzayuni iko wazi kwa walimwengu wote na kuongeza kuwa Waislamu duniani kote wakiwemo Washia na Wasuni wanawajibika kulinda sira ya Mtume wa Uislamu (S.A.W) na Qurani Tukufu na wanapaswa kuwa kitu kimoja dhidi ya maadui.

Ayatullah Kashani amesema kuwa ili kufikia malengo yao, maadui hii leo wanatekeleza mauaji dhidi ya Waislamu, na kwamba licha ya kuwepo fitna na njama zote hizo, lakini Mapinduzi ya Kiislamu na Uislamu wa kweli unaenea kwa kasi kubwa ulimwenguni kote.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo hapa Tehran pia amemtaja Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni muongozo uliosalia wa Jamhuri ya Kiislamu na kueleza kuwa, Kiongozi Muadhamu ni mtu pekee ambaye yuko macho na kutambua vyema njama na malengo ya maadui wa Uislamu; na kwamba huchambua na kubainisha vyema na kwa uwazi siasa za kibeberu kwa watu wote. Ayatullah Muhammad Imami Kashani amesisitiza kuwa Waislamu ulimwenguni hawapasi kuwapuuza maadui wa Uislamu na kuwapa mwanya wa kutimiza malengo yao katika eneo ikiwemo huko Yemen, Iraq na Syria; na kusisitiza kuwa, mauaji na jinai zinazotekelezwa katika nchi hizo, zote hizo zikifadhiliwa na fedha za Saudi Arabia, ni katika kutumikia siasa za Wazayuni na Marekani.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo hapa Tehran ameashiria pia matukio ya hivi karibuni huko Bahrain na kueleza kuwa maulama wa Kishia wanakabiliwa na mashinikizo nchini humo, misikiti inafungwa na wananchi kuteswa; na kwa msingi huo nchi za Kiislamu zinapasa kuzingatia suala hili na kutafuta njia za kukomesha machafuko na ukandamizaji huko Bahrain.

3507725

captcha