
Katika taarifa kwa munasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds, Kamandi ya
Majeshi yote ya Iran imesema, ubunifu wa kistratijia wa Imam Khomeini
MA, katika kuitangaza Ijumaa ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani
kuwa Siku ya Kimataifa ya Qudsn ni fursa kwa ajili ya mapambano dhidi ya
utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ungali changamoto kubwa katika umma
wa Kiislamu.
Wakati huo huo, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran,
Ali Larijani amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono
kikamilifu taifa la Palestina katika mapambano yake dhidi ya utawala wa
Kizayuni."
Larijani ameyasema hayo Jumanne mjini Tehran wakati alipokutana na
wanaharakati kadhaa wanaohusika na mapmabano ya kuikomboa Quds Tukufu na
Palestina kutoka minyororo ya Wazayuni. Larijani amesema kuunga mkono
Palestina ni katika stratijia muhimu za Iran. Larijani amesema Siku ya
Kimataifa ya Quds ni nembo ya azma na irada ya mataifa katika kupigania
ukombozi wa Palestina.
Ijumaa Julai Mosi ni Siku ya Kimataifa ya Quds ambapo watu kutoka
matabaka mbali mbali duniani wanatazamiwa kuandamana na kujumuika kwa
lengo la kufungamana na mapambano ya ukombozi wa Palestina sambamba na
kuulani utawala wa Kizayuni wa Israel na waitifaki wake.
3511039