IQNA

Kadhia ya Palestina

Maandamano makubwa ya Siku ya Kimataifa ya Quds yana umuhimu mkubwa mwaka huu

20:39 - February 18, 2025
Habari ID: 3480232
IQNA-Mkuu wa Makao Makuu ya Intifada na Siku ya Kimataifa ya Quds nchini Iran, Brigedia Jenerali Ramezan Sharif, amesisitiza umuhimu wa kupanga na kufanya juhudi za kufanikisha maandamano makubwa katika Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu.

Kila mwaka, Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, maandamano ya kimataifa hufanyika kwa lengo la kuunga mkono mapambano ya wananchi wa Palestina dhidi ya utawala haramu wa Israel na juhudi za kuikomboa ardhi yao. Ardhi ya Palestina imekuwa ikikaliwa kwa miongo kadhaa na utawala huo.

Siku ya Kimataifa ya Quds ni miongoni mwa urithi ulioachwa na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini, (MA).

Mnamo mwaka 1979, muda mfupi baada ya kuongoza Mapinduzi ya Kiislamu yaliyoangusha utawala wa Shah wa Iran aliyekuwa akiungwa mkono na Marekani, Ayatullah Khomeini alitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Ramadhani kuwa Siku ya Quds.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Tehran, Jenerali Sharif amegusia hali maalum ya mwaka huu, akisema kuwa watu wa Ukanda wa Gaza wamesimama dhidi ya utawala wa Kizayuni kwa mwaka mmoja na nusu na wameonesha kiwango kipya cha mapambano na Muqawama.

Amesema Wapalestina wameonyesha wako tayari kujitoa muhanga kulinda heshima yao na ardhi yao, na wameendelea kushikilia misimamo yao licha ya ukatili wa utawala wa Israel ambao umeua shahidi kwa zaidi ya Wapalestina 50,000 katika kipindi cha miezi 15.

Pia amebainisha kuwa leo, Wamarekani na Waisraeli wanajaribu kutekeleza kile ambacho hawajaweza kufanikisha hadi sasa kwa kupendekeza kuwahamisha wakazi wa Gaza kwa nguvu.

"Kwa mara ya kwanza, wamejumuisha Saudi Arabia na Iraq pamoja na Jordan na Misri katika mpango wa kuwafukuza kwa nguvu wakazi wa Gaza, huku wakizingatia kuwa Syria tayari imekamilika kwao," amesema.

Amesema matukio hayo,  pamoja na ushindi wa mhimili wa Muqawama dhidi ya Wazayuni, vimeunda mazingira tofauti kwa Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu. Afisa hiyo wa Iran amesema anatumai mwaka huu tutashuhudia Siku ya Kimataifa ya Quds yenye tofauti kubwa.

3491910

Habari zinazohusiana
Kishikizo: siku ya quds palestina
captcha