Ayatullah Ahmad Khatami aidha amelaani mashambulizi ya anga ya Jumamosi iliyopita yaliyofanywa na Saudi Arabia kusini mwa Sana'a mji mkuu wa Yemen na kusisitiza kwamba, kuuliwa na kujeruhiwa mamia ya watu kwenye mashambulizi hayo, ni mfano wa wazi wa jinai za kivita na kwamba, watawala wa Saudia wanapasa kupandishwa kizimbani kwa kutenda jinai hizo za kivita.
Imamu wa muda wa Sala ya Ijumaa katika mji wa Tehran ameeleza kuwa, madai yanayotolewa na viongozi wa Marekani na Uingereza kwamba, nchi mbili hizo hazihusiki katika amshambulizi ya Saudi Arabia huko Yemen ni uwongo mtupu. Hii ni kwa sababu, Uingereza ilikuwa tayari imefikia makubaliano ya kuiuzia Saudia silaha za mabilioni ya pesa kabla ya kufanywa shambulio hilo la umwagaji damu la ndege za Saudi Arabia huko Yemen.
Ayatullah Khatami amesisitiza kuwa, uungaji mkono wa Marekani kwa jinai za Saudia nchini Yemen na vile vile kusabisha matatizo kwa nchi nyingine katika eneo hili kwamba ni jambo lisilokubalika na kubainisha kuwa, katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, maelfu ya raia wa Yemen wameuawa, hata hivyo taasisi za kimataifa zimeshindwa kuchukua hatua yoyote ya maana na kuwasilisha malalamiko dhidi ya mauaji hayo ya raia wa Yemen wasio na hatia.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa katika mji wa Tehran pia ameelezea kusikitishwa kwake na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa dhidi ya waombolezaji wa Ta'asua na Ashura mwaka huu huko Iraq na Afghanistan na vile vile kushambuliwa waombolezaji wa Imam Hussein AS nchini Nigeria na kueleza kuwa, maadui wanapasa kufahamu kwamba mapambano ya kumkumbuka Imam Hussen AS yataendelezwa hata katika mazingira magumu kabisa ili kukomesha udhalimu na uistikbari duniani.