IQNA

Kenya kujiunga na OIC na kuanzisha mfumo wa fedha wa Kiislamu

12:14 - January 30, 2016
Habari ID: 3470099
Kenya imeazimia kujiunga na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC sambamba na kuanzisha mfumo wa kifedha wa Kiislamu katika nchi hiyo.
Waziri wa Fedha wa Kenya Henry Rotich ametoa kauli hiyo hivi karibuni na kuongeza kuwa mipango inaendelea kutayarisha ombi la uanachama katika jumuiya hiyo ambayo ni ya pili kwa ukubwa baada ya Umoja wa Mataifa miongoni mwa jumuiya za kiserikali, ikiwa na nchi wanachama 57 zilizoenea kwenye mabara manne makuu ya dunia.
Waziri wa Fedha wa Kenya ameyasema hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari baada ya kuongoza ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Kiislamu wa Fedha uliofanyika jijini Nairobi.
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ambayo inashughulikia zaidi maslahi ya mataifa ya Waislamu ina uhusiano wa kiushauri na kiushirikiano na Umoja wa Mataifa katika kutatua mizozo na migogoro inayohusisha nchi wanachama.
Ili nchi iweze kupata mikopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kiislamu (IDB) yenye makao yake makuu mjini Jeddah, Saudi Arabia, inapaswa kuwa mwanachama wa OIC.
Akizungumzia nukta hiyo, Waziri wa Fedha wa Kenya amesema: "IDB imezipatia mikopo nchi nyingi za Afrika za eneo la Jangwa la Sahara, lakini Kenya bado haijawa mwanachama. Mara tu tutakapojiunga na OIC tutaweza kupata tahafifu kubwa za masuala ya fedha kama tunavyofanyiwa na Benki ya Dunia.”
Rotich amebainisha kuwa: "Kenya itaanza kutumia mkompo wa dhamana sukuk kuanzia mwaka ujao." Rotich amongeza kuwa Kenya inaweza kunufaika na mfumo wa kifedha wa Kiislamu kwa kupata ushauri kutoka nchi za Kiislamu. Kongamano hilo la Nairobi lilikusudia kuzisaidia nchi za Afrika kunufaika na soko kubwa la  mfumo wa Kiislamu wa kifedha duniani unaoamnikiwa kuwa na thamani ya dola trilioni 2.1.  Washiriki wa kongamano hilo la Jumapili na Jumatatu iliyopita walisisitiza kuhusu kutumika mfumo wa fedha wa Kiislamu kukabiliana na umasikini barani Afrika.
3471225

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha