IQNA

Bunge la Ufilipino Laidhinisha Siku ya Kitaifa ya Hijabu

13:33 - October 02, 2017
Habari ID: 3471201
TEHRAN (IQNA)-Bunge la Ufilipino limepitisha muswada wa sheria ya kutangaza tarehe mosi Februari kila mwaka kuwa Siku ya Kitaifa ya Hijabu nchini humo.

Kamati ya masuala ya Waislamu katika bunge hilo imeidhinisha pendekezo hilo la mbunge Bi. Sitti Djalia A Turabin-Hataman (kwenye picha).

Katika kutetea pendekezo lake, mbunge huyo amesema wanawake Waislamu wanaovaa Hijabu kote duniani wanaendelea kubaguliwa na kubughudhiwa na hivyo kuna haja ya kuelimisha jamii kuhusu vazi hilo.

"Kuvaa Hijabu ni haki ya kila mwanamke Mwislamu. Si kipande cha nguo bali ni mfumo wa maisha yake. Katika Qur’ani Tukufu, wanawake wote Waislamu wametakiwa wajisitiri na wasiwe ni wenye kuonyesha mapambo yao,” aliongeza kusema.

Siku ya Hijabu Duniani iliadhimishwa kwa mara ya kwanza Februari Mosi mwaka 2013 kufuatia pendekezo la Nazma Khan kama njia ya kukabiliana na chuki dhidi ya Hijabu.

Mbunge Turabin-Hataman amesema Siku ya Hijabu Duniani sasa huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kuwahimiza wanawake Waislamu na wasiokuwa Waislamu kuvaa vazi hilo la stara la Kiislamu.

"Wanawake wanaovaa Hijabu wanakabiliwa na changamoto nyingi kote duniani. Kuna ripoti kuwa Waislamu wanaovaa Hijabu wanakandamizwa na kubaguliwa. Kwa mfano nchini Marekani baada ya matukio ya 9/11, wanawake Waislamu wanaovaa Hijabu wamekuwa wakibaguliwa na kuhujumiwa,” aliongeza.

Mbunge huyo aidha amebainisha masikitiko yake kuwa baadhi ya vyuo vikuu Ufilipino vimewazuia wanafunzi Waislamu kuvaa Hijabu na hivyo kuwalazimisha baadhi kuacha masomo. Amesema hatua kama hizo ni ukiukwaji wa uhuru wa kuabudu. Aidha amesema Siku ya Kitaifa ya Hijabu Ufilipino inalenga kuondoa ile dhana potovu kuwa vazi la Hijabu ni nembo ya kukandamizwa, ugaidi au kokosa uhuru. Ameongeza kuwa analenga kusitisha ubaguzi wanaotendewa wanawake Waislamu wanaovaa Hijabu sambamba na kuleta maelewano na kuheshimiana miongoni mwa Wafilipino wa tamaduni na dini mbali mbali ili kudumisha umoja na amani nchini hum.

Ufilipino ni nchi iliyo katika Asia ya Kusini-Mashariki na idadi ya watu nchini humo inakadiriwa kuwa milioni 103 ambapo karibu asilimia 80 ni Wakatoliki na takribani asilimia 12 ni Waislamu.

3648130

captcha