IQNA

13:37 - April 29, 2019
News ID: 3471934
TEHRAN (IQNA)- Mkuu wa Tume ya Kiislamu ya Haki za Binadamu (IHRC) Massoud Shajareh amesema utawala wa Nigeria hauna budi ila kumuachilia huru kiongozi wa harakati ya Kiislamu nchini humo Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Kufuatia jitihada za IHRC, serikali ya Nigeria hivi karibuni iliruhusu timu ya madaktari kumtembelea na kumfanyia uchunguzi wa kitiba Sheikh Zakzaky na mke wake wanashikiliwa katika kizuizi cha serikali ya Nigeria.

Katika mahojiano maalumu na IQNA, Shajareh amebainisha masikitiko yake kuwa serikali ya Nigeria inamshikilia Sheikh Zakzaky na mke wake Bi. Zeenah Ibrahim.

Amesema Mahakama ya Kilele nchini Nigeria iliamuri Sheikh Zakzaky aachiliwe huru na hivyo kuendelea kushikiliwa mwanazuoni huyo na mke wake ni kinyume cha sheria.

Shajareh amesisitiza kuwa, ni vigumu kwa wawili hao kupata huduma maalumu za kitiba wakiwa kizuizini kutokana na vizingiti vinavyowekwa na serikali. Aidha amesema kwa ujumla hakuna suhula zinazofaa za kitiba nchini Nigeria kuwapata matibabu wawili hao ambao wana majeraha ya risasi.

Hatimaye Aprili 26 timu ya madaktari iliruhusiwa kumfanyia uchunguzi wa kiafya Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambaye angali anashikiliwa kizuizini.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepongeza na kukaribisha kwa mikono miwili hatua ya serikali ya Nigeria ya kuruhusu Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria kutembelewa na timu ya madaktari.

Sayyid Abbas Mousavi amesema kuwa, hatua na uamuzi huo wa serikali ya Nigeria ni chanya na kwamba, Tehran inapongeza na kukaribisha uamuzi huo wa kuruhusu timu ya madaktari kuonana na Sheikh Zakzaky pamoja na mkewe.

IHRC: Nigeria haina budi ila kumuachilia huru Sheikh Zakzaky

Masoud Shajareh na madaktari waliomtembelea Sheikh Zakzaky

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, ana matumaini kwamba, kutibiwa kikamilifu Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe nje au ndani ya Nigeria kutaandaa uwanja wa ushirikiano na mazungumzo mazuri baina ya viongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria na serikali ya nchi hiyo na hivyo kuachiliwa huru mwanaharakati huyo wa Kiislamu.

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walikamatwa na kuwekwa kizuizini tarehe 13 Desemba 2015, wakati askari wa jeshi la Nigeria walipovamia na kufanya hujuma dhidi ya Hussainiyyah ya mji wa Zaria katika jimbo la Kaduna kaskazini mwa nchi hiyo, ambapo mamia ya Waislamu waliuawa shahidi.

3806996

Name:
Email:
* Comment: