IQNA

12:35 - June 29, 2019
News ID: 3472021
TEHRAN (IQNA)- Baada ya kupita miaka mitatu na nusu tangu serikali ya Nigeria ianze kumshikilia kinyume cha sheria Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky na kuendelea kukaidi amri ya Mahakama Kuu ya kuachiliwa huru mwanachuoni huo, hivi sasa hali ya kiongozi huyo wa Waislamu imezidi kuwa mbaya.

Uchunguzi mpya wa madaktari unaonesha kuweko chembechembe za sumu katika damu ya Sheikh Zakzaky suala ambalo linathibitisha kuwa amepewa sumu akiwa jela. Baada ya hali ya Sheikh Zakzaky na mkewe kuzidi kuwa mbaya, kwa mara nyingine Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imetoa mwito wa kuachiliwa huru, lakini Mahakama Kuu ya jimbo la Kaduna inaendelea kuweka pingamizi licha ya Mahakama Kuu ya Nigeria kutoa amri aachiliwe huru. 

Tarehe 13 Disemba 2015, Sheikh Zakzaky alitekwa na wanajeshi wa Nigeria baada ya kupigwa risasi yeye na mkewe katika mji wa Zaria wa jimbo la Kaduna. Baada ya kupita mwaka mmoja, yaani mwezi Disemba 2016, Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa amri ya kuachiliwa huru Zakzaky baada ya kuthibitisha kuwa hana hatia na ilitoa amri kwa jeshi na taasisi za usalama za Nigeria kuilipa familia ya Sheikh Zakzaky fidia ya dola laki moja na 50 elfu. Hata hivyo jeshi na serikali ya Nigeria zimekataa kutekeleza amri hiyo ya Mahakama Kuu na mpaka sasa hivi anaendelea kushikiliwa korokoroni. Ukaidi huo wa jeshi na serikali ya Nigeria umepelekea hali ya Sheikh Zakzaky kuzidi kuwa mbaya na wakati huo huo umechochea hasira za Waislamu wa Nigeria ambao hadi leo hii wanatumia matukio tofauti kuonesha upinzani wao dhidi ya dhulma anayofanyiwa mkuu huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria. Maafisa wa mahakama katika jimbo la Kaduna nao wanachangia kutoachiliwa huru Sheikh Zakzaky licha ya kwamba hali yake na mkewe inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku.

Katika taarifa yake ya karibuni kabisa, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imesema Ijumaa tarehe 28 Juni 2019 kwamba, inahuzunishwa mno na hali mbaya ya kiafya ya Sheikh Zakzaky na mkewe na imetangaza kuwa kitendo cha serikali kuu ya Nigeria cha kukataa kuwaachilia huru yeye na mkewe ili waende wakatibiwe nje ya nchi, ni uvunjaji wa wazi wa haki za binadamu na kuna uwezekano lengo kuu la serikali ya Nigeria ni kumuua kwa siri mwanachuoni huyo. 

Kitendo cha serikali ya Nigeria cha kutowaruhusu madaktari kumuangalia na kumtibu Sheikh Zakzaky kimewafanya viongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo kusema muda mrefu sasa kwamba lengo hasa la serikali ya Nigeria ni kumuua kiongozi wao huyo. Hivi karibuni harakati hiyo ya Kiislamu ilitoa ufafanuzi kuhusu hali mbaya ya kiafya ya Sheikh Zakzaky na kusisitiza kwamba baadhi ya madola ya kigeni yanaishinikiza serikali ya Nigeria isimwachilie huru mwanachuoni huyo hadi itakapomuua shahidi.

Kwa muda mrefu sasa Saudi Arabia na baadhi ya waitifaki wake wanafanya njama za kujipenyeza barani Afrika. Misaada ya siri na ya dhahiri ya kifedha na kijeshi kwa nchi za Afrika ni miongoni mwa njia zinazotumiwa na Saudia ili kuzirubuni nchi za baraza hilo zifuate siasa za Riyadh. Nigeria nayo ni nchi yenye Waislamu wengi zaidi barani Afrika hivyo inapewa mazingatio makubwa na Saudi Arabia. Katika upande mwingine, utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya kampeni kubwa ya kuwa na ushawishi barani Afrika kama zilivyo nchi za kikoloni za Magharibi. Madhalimu hao wanazilenga sana nchi zenye Waislamu wengi kama Nigeria ili kuzidi kuonesha chuki zao dhidi ya Waislamu.

Akizungumzia suala hilo, Sheikh Adam Soho, mmoja wa wanachama waandamizi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria anasema, serikali ya Nigeria imeathiriwa sana na siasa za madola ya Saudia, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, na wote hao wanashirikiana kuendesha njama na uadui dhidi ya Waislamu hasa Waislamu wa Kishia. 

Inaonekana wazi kwamba kuna mizozo na mivutano mikubwa baina ya Waislamu wa Nigeria na serikali ya nchi hiyo na hivi sasa mzozo mkubwa uliopo baina ya pande hizo umejikita kwenye imma kumuua au kumwachilia huru mwanachuoni huyo mwanaharakati, Sheikh Ibrahim, Zakzaky.

Abu Hamid, mmoja wa wanachama waandamizi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema: Serikali ya Abuja ina nia ya kumuua shahidi Sheikh Zakzaky kwa mashinikizo ya Saudi Arabia. 

3468854

 

Name:
Email:
* Comment: