IQNA

15:29 - May 19, 2019
News ID: 3471964
TEHRAN (IQNA) – Muungano wa kivita unaoonogzwa na Saudi Arabia umebomoa zaidi ya misikiti 1,024 tangu uanzishe vita dhidi ya Yemen mwaka 2015, amesema afisa wa ngazi za juu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen.

Katika mahojiano na IQNA akiwa katika Maonyesho ya 27 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Tehran, Bw. Adnan Qafla, afisa wa ngazi za juu wa masuala ya kigeni katika Harakati ya Ansarullah amesema kati ya misikiti ambayo imebomolewa katika hujuma za Saudi na waitifaki wake dhidi ya Yemen ni misikiti iliyojengwa na maswahaba wa Mtume SAW na Maimamu Watoharifu AS.

Ameongeza kuwa, idadi kubwa ya nakala za Qur'ani Tukufu pia zimeharibiwa au kuteketea moto katika mashambulizi ya mabomu ya muungano wa kivita wa Saudia dhidi ya misikiti ya Yemen.

Qafla amesema kubomolewa misikiti na kuharibiwa misahafu ni kati ya jinai mbaya zaidi ambazo zimetendwa na muungano huo unaoongozwa na Saudi Arabia lakini akasisitiza kuwa Wayemen watasimama imara na wataendeleza mapambano kutokana na Imani yao kwa Qur'ani Tukufu na Ahul Bayt AS.

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha usukani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.

Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasio na hatia. Zaidi ya watu 16,000 wanaripotiwa kupoteza maisha katika vita vya Saudia dhidi ya Yemen. Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani na utawala haramu wa Israel.

/3812578/

Name:
Email:
* Comment: