IQNA

19:25 - September 20, 2019
News ID: 3472140
TEHRAN (IQNA) – Misikiti 44 kote Afrika Kusini itafungua milango wazi kwa umma mnamo Septemba 24 katika Siku ya Turathi, ambayo lengo lake ni kuleta maelewano ya kijamii na kuunda taifa lenye kuwajumuisha wote katika nchi hiyo.

Katika taarifa, Dkt. Faisal Suliman, Mwenyekiti wa Mtandao wa Waislamu Afrika Kusini (SAMNET) amesema, "Katika Siku ya Turathi, watu wa Afrika Kusini hujumuika na kujifunza kuhusu tamaduni za wengine, na kusherehekea historia yao ya pamoja na namna ambavyo jamii imeweza kuwa jumuishi."

Amesema katika kufikia lengo la jamii jumuishi, Siku ya Kitaifa ya Milango Wazi Misikitini huwa ni jukwaa la kuwawezesha wasiokuwa Waislamu kuingia katika msikiti na kujifunza kuhusu Uislamu kutoka kwa Waislamu.

Amesema katika siku hiyo wasiokuwa Waislamu hukutana na Waislamu na kutembezwa katika msikiti na kisha kufahamishwa kuhusu maudhui kama vile Sala, wudhuu na Hijabu na baada ya hapo hufanyika kikao cha kuuliza na kujibiwa maswali kuhusu Uislamu na Waislamu.

Mwaka 2018 katika Siku ya Kitaifa ya Milango Wazi Misikitini takribani wageni 800 wasiokuwa Waislamu walitembelea misikiti 20 katika mikoa minne Afrika Kusini na waliweza kujifunza mengi.

Siku ya Turathi, ambayo inajumuisha Siku ya Kitaifa ya Milango Wazi Misikitini, inasherehekewa kumuenzi Mfalme wa Wazulu, Shaka, ambaye alikuwa mstari wa mbele kuleta umoja Afrika Kusini.  Kila mwaka watu hujumuika katika kaburi la Mfalme Shaka kumuenzi katika siku hiyo kutokana na jitihada zake za kuliunganisha taifa la Afrika Kusini.

Waislamu nchini Afrika Kusini wanakadiriwa kuwa ni asilimia 2 ya watu wote milioni 55 nchini humo.

3843419

Name:
Email:
* Comment: