IQNA

Uhasama mkubwa wa kisiasa Marekani, Trump akataa kumpa mkono Pelosi, naye aichana hotuba yake

11:35 - February 05, 2020
Habari ID: 3472442
TEHRAN (IQNA)- Mgawanyiko mkubwa umedhihirika katika uga wa kisiasa Marekani wakati rais Donald Trump wa nchi hiyo alipokuwa akitoa hotuba ya kila mwaka mbele ya Bunge la Kongresi huku mchakato wa kumuondoa madakarani ukikaribia kumalizika.

Wakati Trump alipopanda kwenye jukwaa, alimpuuza na kukataa kumpa mkono Spika wa Baraza la Wawakilishi katika Bunge la Kongresi Nancy Pelosi ambaye alikuwa amemnyooshea mkono.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza Trump kukutana uso kwa uso na Pelosi ambaye ni hasimu wake mkuu wa kisiasa anayeongoza mchakato wa Wademocrat wa kumuuzulu.

Katika hotuba yake, Trump alikituhumu chama cha Democrat kwa kupanga kuwalazimisha walipa kodi wa Marekani kutoa huduma ya afya ya bure kwa wahamiaji wasio na nyaraka, Pelosi alionekana mara mbili akisema: "Sio kweli."

Pelosi, ambaye ni kinara wa chama cha upinzani cha Demokrat, alionekana mwenye hasira wakati wa hotuba ya Trump ambapo alirarua nakala ya hotuba hiyo na kuitupa mezani.

Trump ambaye hakutaja kadhia  ya kumuuzulu katika hotuba yake alikuwa akishangiliwa mara kwa mara na wabunge wa chama chake cha Republican.

Siku ya Jumatano Baraza la Senate, ambalo linadhibitiwa na Warepublican, litapiga kuru kuhusu iwapo Trump ataondolewa ofisini au la. Inatazamiwa kuwa Trump hatauzuliwa kwani Warepublican 53 katika baraza wameonekana kupinga wazi mchakato huo wa Wademokrat.

3876656

captcha