Valentina Gomez, ameibua hasira kali baada ya kuonekana kwenye video akitangaza kile alichokitaja kuwa "vita dhidi ya Uislamu na Waislamu." Katika mkanda huo Gomez anaonekana akichoma moto nakala ya kitabu kitukufu cha Qur'ani na kusema, "Nitaangamiza Uislamu. Nisaidie kushinda uchaguzi."
Kitendo hicho kimezua ukosoaji mkubwa na hisia za hasira dhidi ya mgombea huyo wa chama cha Rais Donald Trump katika uchaguzi wa Kongresi ya Marekani. Wengi wameishutumu kampeni yake ya kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa lobi ya Wazayuni kwa kufanya uchochezi dhidi ya Waislamu, wakiamini kwamba kushambulia Uislamu imekuwa sharti la kupata msaada wa kifedha na kilojistiki kutoka kwa lobi hiyo ya Wazayuni.
Baadhi ya wanablogu waliochukizwa na kitendo hicho wamehoji kwamba: Je, wito wa Valentina Gomez, mgombea ubunge kutoka Texas, sio kuchochea chuki, vurugu, na uadui wa waziwazi dhidi ya uhuru wa kufuata dini kwa mujibu wa kanuni za haki za binadamu na Katiba ya Marekani, suala ambalo ni uhalifu unaoadhibiwa na sheria? Kwa nini Gomez hawajibishwi kisheria kwa mwenendo huu wa uchochezi?
Wengine wamekosoa kile walichokitaja kuwa ni sera na misimamo ya kinafiki na kindumakuwili, wakieleza kwamba majukwaa na vyombo vya sheria huchukua hatua haraka na madhubuti dhidi ya matamshi yoyote ya chuki yanayolenga Wayahudi au kundi lolote linalolindwa, na kinyume chake, yanakaa kimya dhidi ya hujuma dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Wakosoaji wengi wamesisitiza kuwa, matamshi ya kutaka Uislamu uangamizwe si tu "misimamo mikali," bali ni vita vya wazi vya kifikra na uchochezi dhidi ya dini na wafuasi wake.
Wanasema, kupuuza matamshi hayo kunatengeneza mazingira ya uhalifu wa chuki dhidi ya Waislamu, na kunatoa ujumbe kwamba Uislamu na Waislamu wanaweza kuchambuliwa bila kuchukuliwa hatua, jambo ambalo linatoa changamoto kwa hisia za Waislamu zaidi ya bilioni mbili duniani.
Kuongezeka kwa Uhasama Dhidi ya Uislamu
Video ya Gomez ya kuteketeza moto nakala ya Qur’an inatokea wakati ambapo uhasama dhidi ya Waislamu unaongezeka sehemu mbalimbali za dunia, ikiwemo Marekani. Makundi ya utetezi wa Waislamu yanasema hotuba za chuki na matukio dhidi ya Waislamu yameongezeka, hasa miongoni mwa wanasiasa wa mrengo wa kulia mkali.
Katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya wanasiasa na wagombea wa Republican wametumia hotuba za kupinga Waislamu kuwavutia baadhi ya wapiga kura. Hii imezidisha migawanyiko nchini Marekani.
Tukio hili pia linafanana na migogoro kama hiyo Ulaya. Katika Uswidi, wanaharakati wa mrengo wa kulia walifanya maandamano na kuteketea moto nakala ya Qur’an nje ya misikiti mnamo 2023 na 2024, jambo ambalo liliibua maandamano katika nchi nyingi za Kiislamu.
Serikali ya Uswidi ilishutumu matendo hayo lakini ilidai yanaungwa mkono na sheria za uhuru wa maoni.
Waislamu wengi, ndani na nje ya Marekani, wanayaona matendo kama haya si uhuru wa maoni bali ni mashambulizi ya makusudi dhidi ya imani na utambulisho wao. Makundi ya utetezi yanasema kulinda uhuru wa dini kunamaanisha kuhakikisha hakuna jamii inayolengwa kwa chuki.
3494395