IQNA

Mkakati wa utawala wa Kizayuni wa kueneza satwa yake ya kibeberu barani Afrika

14:39 - February 06, 2020
Habari ID: 3472445
TEHRAN (IQNA) - Ikiwa ni katika kuendeleza juhudi zake kueneza satwa ya kibeberu na kutafuta washirika kwa minajili ya kutekeleza siasa zake za kivamizi, Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala haramu amekutana na kufanya mazungumzo mjini Entebbe Uganda na Luteni Jenerali Abdul-Fattah al-Burhan, Kiongozi wa Baraza la Utawala la Sudan.

Mazungumzo hayo kati ya Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kiongozi wa baraza kuu la utawala la Sudan yalipangwa yawe ya siri kiasi kwamba, Asma Mohamed Abdalla, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan alitangaza kuwa, hana taarifa yoyote kuhusiana na mazungumzo hayo. Hata hivyo Benjamin Netanyahu ameweka wazi mazunguzmo hayo ya Jumatatu wiki hii na kuandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Nimekutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi wa Baraza la Utawala la Sudan na kujadiliana naye kuhusiana na suala la kufanywa kuwa wa kawaida uhusiano wa Tel Aviv na Khartoum.

Uwepo wa siri na dhahiri

Kwa miaka mingi sasa utawala haramu wa Israel umekuwa ukilizingatia bara la Afrika katika siasa na ushawishi wake na umekuwa na uwepo wa siri na dhahiri katika medani mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kiusalama katika nchi tofauti za bara hilo.

Katika miaka ya hivi karibuni kutokana na mabadiliko yaliyotokea katika nyanja mbalimbali za jiopotiki ulimwenguni na kadhalika siasa za uungaji mkono wa upande mmoja za Rais Donald Trump wa Marekani, juhudi za viongozi wa Israel za kuongeza upenyaji na ushawishi wake katika nchi mbalimbali barani Afrika na kupata washirika na waitifaki kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la malengo yake zimeshika kasi mno.

Sudan ni miongoni mwa nchi muhimu na zinazolengwa na viongozi wa Israel. Kwa miaka mingi viongozi wa Tel Aviv walikuwa wakitaka kuifanya Sudan iwe pamoja na Tel Aviv katika siasa zake. Mchango wa siri wa Israel katika kujitenga Sudan Kusini na Sudan, kuchochea hitilafu za ndani katika nchi hiyo na vita vya Darfur ni miongoni mwa hatua za Wazayuni katika uwanja huo. Katika miezi ya hivi karibuni pia kuvurugika anga ya kisiasa ya Sudan, kulichangiwa na utawala wa Saudi Arabii ikiwa mshirika wa mchezo mchafu wa Israel katika eneo, ambapo viongozi wa Aal Saud walikuwa na nafasi katika uwanja huo.

Sudan yalengwa

Hivi sasa Waziri Mkuu wa Israel ametangaza bayana kwamba, ameingia uwanjani kwani kustafidi na Sudan kiuchumi na kisiasa ni jambo ambalo limekuwa na umuhimu kwa utawala huo ghasibu. Katika uga wa siasa kwa miongo mingi Sudan ilijitenga mbali na Israel na kuwa pamoja na Wapalestina kwa ajili ya kutetea na kulinda matukufu ya wananchi hao madhulumu.

Lakini katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kuongezeka lobi za Wazayuni na uingiliaji wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja wa Israel, mkondo wa kisiasa wa Sudan umebadilika ambapo kutokana na nchi hiyo kukabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi, hitajio la fedha, kuongezeka pengo la hitilafu za kimitazamo baina ya vyama na makundi ya kisiasa sambamba na kuathirika na siasa za Aal Saud, nchi hiyo ya Kiafrika imeipatia Israel ishara ya ridhaa.

Kadhia ya Muamala wa Karne imegeuka na kuwa msukumo kwa Benjamin Netanyahu wa kutafuta ridhaa na mwafaka wa viongozi wa Khartoum kuhusiana na mpango huu wa kidhalimu.

Usaliti kwa taifa la Palestina

Saeb Erekat, Katibu wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: Kukutana Luteni Jenerali Abdul-Fattah al-Burhan, Kiongozi wa Baraza la Utawala la Sudan na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ni usaliti kwa taifa la Palestina na kujiondoa waziwazi katika ubunifu wa amani ya Kiarabu.

Kunufaika na uchumi na vyanzo vya utajiri wa madini wa Sudan na kadhalika nafasi ya nchi hiyo ni malengo mengine ya viongozi wa Israel katika kipindi cha hivi sasa, kiasi kwamba, kiongozi mmoja aliyeandamana na Netanyahu katika safari yake hiyo amesema kuwa, jambo la kwanza lenye faida kwa Tel Aviv ni kupata idhini ya kupita ndege za Israel katika anga ya Sudan.

Licha ya kuwa juhudi Waziri Mkuu wa Israel za kuwa na ushawishi barani Afrika zimeongezeka, lakini akthari ya wananchi wa bara hilo hawakubaliani na utendaji huo bali wanafungamana kikamilifu na malengo yao matukufu. Baada ya mazungumzo ya Luteni Jenerali Abdul-Fattah al-Burhan na Netanyahu ambayo yalipangwa yawe ya siri, hatua ya kutangazwa mazungumzo hayo na hata vipengee vya mazungumzo yenyewe kuelezwa hadharani, kumewafanya viongozi wa Sudan wahofie radiamali za baadaye. Wasiwasi na woga huo ndio ulioifanya serikali ya Khartoum itangaze kuwa, al-Burhan amekutana na kufanya mazungumzo na Netanyahu bila ya kulishauri wala kulijulisha Baraza la Mawaziri ,na hivi sasa sisi tunasubiri maelezo kutoka kwa kiongozi huyu kuhusiana na jambo hili.

Al Burhan hasamehewi

Kwa kuzingatia himaya na uungaji mkono wa wananchi wa Sudan kwa malengo matukufu ya Palestina na licha ya kufanyika mazungumzo baina ya Burhan na Netanyahu, lakini haionekani kama Israel itaweza kuwa na nafasi muhimu ya hivyo katika nchi hiyo, hasa kwa kuzingatia kuwa, mazungumzo hayo yamekabiliwa na ukosoaji mkubwa pia katika ulimwengu wa Kiarabu. Ali al-Houthi, mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa nchini Yemen sambamba na kukosoa kukutana al-Burhan na Netanyahu amesema kuwa, sidhani kama wananchi wa Sudan watamsamehe Abdul-Fattah al-Burhan kwa kitendo chake hicho.

3876817

captcha