IQNA

Rais Hassan Rouhani

Mapinduzi ya Kiislamu ni chaguo la taifa zima la Iran

20:16 - February 11, 2020
Habari ID: 3472461
TEHRAN (IQNA) - Rais Hassan Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kustawi na kuimarika licha ya uhasama na njama za maadui hususan Marekani, na kwamba 'Mapinduzi ya Kiislamu' lilikuwa chaguo la taifa zima la Iran.

Rais Rouhani amesema hayo leo akiwahutubia wananchi wa Iran katika maadhimisho ya miaka 41 ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Medani ya Azadi hapa jijini Tehran na kufafanua kuwa, Marekani kwa miaka 41 sasa inaendelea kuota ndoto za kurejea Iran lakini wananchi wa Iran walichukua uamuzi wa kuwa na Jamhuri ya Kiislamu, jambo ambalo linawaghadhabisha watawala wa Washington.

Amesema kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu, Iran ilikuwa ikiagiza kutoka nje asilimia 95 ya silaha, lakini hii leo taifa hili linajitosheleza katika nyuga za kijeshi, sayansi na teknolojia kwa kutegemea ujuzi wa wataalamu wa hapa nchini.

Amebanisha kuwa, taifa la Iran lisingechagua Mapinduzi ya Kiislamu iwapo tawala za kidikteta zilizopita zingewapa uhuru wa kuchagua viongozi wanaowataka, kuwa na katiba wanayoitaka pamoja na kuwa na chaguzi huru na za haki.

Huku akiashiria athari chanya za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa nchi za eneo, kwa Waislamu na wapenda haki kote duniani, Rais Rouhani amebainisha kuwa, "Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zinatambua vyema nguvu za Mapinduzi ya Kiislamu, na ndiposa daima zimekuwa zikishadidisha uadui na chuki zao dhidi ya taifa la Iran."

Ameongeza kuwa, sera ghalati za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu hazijawa na athari hasi kwa eneo hili tu, bali hata kwa Wamarekani wenyewe.

Kwingineko katika hotuba yake mbele ya mamilioni ya Wairani waliokusanyika katika Medani ya Azadi hapa Tehran, Dakta Rouhani amebainisha kuwa, diplomasia na muqawama ni silaha mbili za kupambana na adui. Amesema, "Shahidi Soleimani alikuwa Jenerali katika medani za vita na pia mwanadiplomasia wa ngazi za juu katika mazungumzo ya kidiplomasia katika eneo. Aliuawa shahidi akielekea kuonana na Waziri Mkuu wa Iraq na wala sio katika uwanja wa vita."

Amesisitiza kuwa, Marekani na Israel zinabwabwaja na kuwahadaa walimwengu kumhusu Shahidi Soleimani, lakini ni wazi kuwa Kamanda Mkuu huyo wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikuwa anapigana kufa kupona kuhakikisha kuwa eneo hili la Asia Magharibi linakuwa na usalama na uthabiti.

Kadhalika Rais Hassan Rouhani amewaasa wananchi wa Iran kudumisha umoja na mshikamano wao sambamba na kushiriki kwa wingi katika uchaguzi ujao wa Bunge.

3878098

captcha