IQNA

Iran yaionya vikali Israel kuhusu uchokozi, vitisho

8:13 - February 13, 2020
Habari ID: 3472466
TEHRAN (IQNA) - "Iwapo utawala wa Kizayuni wa Israel utatekeleza uvamizi au hatua yoyote ya kijinga dhidi ya maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Syria na katika eneo, basi utawala huo utapokea jibu kali ambalo litakuwa la majuto."

Hiyo ni kauli ya Sayyid Abbas Mousavi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kufuatia madai na vitisho vya afisa mmoja wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Katika taarifa aliyotoa Jumatano, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa: "Msingi na utambulisho wa utawala huo katika kipindi cha miaka 70 ya kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina na nchi jirani umekuwa ni mauaji, uporaji mali, ugaidi na uvamizi."

Mousavi ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko nchini Syria kufuatia mwaliko rasmi na mapatano na serikali ya nchi hiyo kwa lengo la kukabiliana na magaidi wanaopata himaya ya Marekani na Israel. Ameongeza kuwa, Iran katu haitasita au kulegea hata lahadha moja katika kulinda uwepo wake Syria na katika kutetea usalama wake wa kitaifa na maslahi yake katika eneo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa  Iran itafuatilia vitisho na matamshi ya kutaka vita ya utawala ghasibu wa Israel katika taasisi za kimataifa.

Naftali Bennett, Waziri wa Vita wa Utawala wa Kizayuni amekariri madai yasiyo na msingi yaliyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kusema Israel daima inatekeleza jitihada za kuidhoofisha Iran ili kuilazimisha iondoke Syria.

Mgogoro wa Syria uliibuka mwezi Machi 2011 baada ya makundi mengi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudi Arabia, Imarati, Marekani, utawala haramu wa Israel na washirika wao kuivamia nchi hiyo kwa lengo la kubadili mlingano katika eneo la Asia Magharibi kwa maslahi ya utawala huo wa Kizayuni.

Hata hivyo, msimamo imara wa serikali ya Damascus chini ya uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na washirika wake, umeweza kufelisha njama hizo za maadui sambamba na kuyashinda makundi hayo ya kigaidi.

3878502

captcha