IQNA

Ugonjwa wa corona wazidisha chuki dhidi ya Waislamu India

12:10 - April 04, 2020
Habari ID: 3472631
TEHRAN (IQNA) – Ugonjwa wa COVID-19 au corona umepelekea kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu nchini India.

Wakuu wa serikali ya India wamedai kuwa kesi nyingi za COVID-19  nchini humo zimetokana  mjumuiko wa kila mwaka wa Waislamu (Ijtimai)  ambao ulifanyika New Delhi mapema mwezi Machi. Maafisa wa afya nchini India sasa wanawafuatilia watu wote walioshiriki au waliokaribiana na washiriki wa kongamano hilo.

Chuki hizo  dhidi ya Waislamu zimekuja wiki kadhaa baada ya makumi ya Waislamu India kuuawa katika hujuma zilizotekelezwa na Wahindu wenye misimamo ya kufurutu ada pamoja na maafisa wa usalama nchini humo.

Wakati huo huo Maulana Badruddin, mbunge katika bunge la India amesema kuwa, serikali ya nchi hiyo inatumia vibaya virusi vya Corona kama wenzo wa kuwakandamiza Waislamu.

Badruddin Ajmal aliyasema hayo Alkhamisi ambapo sambamba na kukosoa siasa za serikali ya India za kuwalenga Waislamu wa nchi hiyo, amesema kuwa, hatua ya kuwatuhumu Waislamu kuwa ndio walioeneza virusi vya Corona ndani ya nchi hiyo, haina ushahidi wowote na pia kwamba ni kinyume na maadili. Mbunge huyo ambaye pia ana nafasi muhimu ya kidini nchini India ameongeza kwa kusema: "Tunashuhudia ushetani wa baadhi ya vyombo vya habari dhidi ya Waislamu ambapo vinajaribu kuhusisha uwepo wa virusi vya Corona katika kituo cha jumuiya moja ya ulinganiaji mjini New Delhi na kuenea kwake nchini humo, jambo ambalo kwa hakika ni kosa kubwa." 

Maulana Badruddin Ajmal amebainisha kwamba, serikali ya India inafahamu vyema kwamba Jumuiya ya Tablighi inajihusisha tu na masuala jumla ya maisha ya watu lakini pamoja na hayo haijazuia kuenezwa habari hizo za uongo dhidi ya Waislamu. Wizara ya Afya ya India imetangaza kuwa, hadi sasa nchi hiyo ina waathirika 3,082 wa Corona na kwamba 86 kati yao tayari wamepoteza maisha katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.

3471031

captcha