IQNA

Iran iko tayari kwa hali yoyote itakayojitokeza kuhusu ibada ya Hija mwaka huu

19:38 - April 07, 2020
Habari ID: 3472643
TEHRAN (IQNA) – Mkuu wa Idara ya Hija na Ziyara ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelezea matumaini yake kuwa, janga la COVID-19 au corona litamalizika utakapowadia msimu wa joto na kwamba Hija itafanyika kama ilivyopangwa. Hatahivyo ameongeza kuwa, Iran iko tayari kwa hali yoyote itakayojitokeza kuhusu Ibada ya Hija mwaka huu.

Ali Ridha Rashidian Mkuu wa  Idara ya Hija na Ziyara ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema iwapo janga la la COVID-19 litamalizika na uamuzi ukachukuliwa kuhusu kuendelea na Ibada ya Hija, Iran itatuma wananchi wake kutekeleza ibada hiyo kwa kuzingatia masharti yote, hasa ya afya ya mahujaji.

Amesema hivi sasa Iran inaendeleza mashauriano na Saudi Arabia kuhusiana na ibada ya Hija mwaka huu.  Aidha amesema Iran inaongoza jitihada za ushirikiano baina ya nchi za Kiislamu kuhusu kuandaa Ibada ya Hija kwa kuzingatia ulindwaji afya ya Mahujaji. 

Halikadhalika amesema iwapo janga la COVID-19 litaendelea na Saudia Arabia iamue kuwa Ibada ya Hija itaendelea, wale ambao wako katika hatari ya juu ya kuambukizwa ugonjwa huo hawataruhusiwa kuelekea katika ardhi takatifu za Makka na Madina.

Bw. Rashidian pia amesema iwapo Ibada ya Hija haitafanyika mwaka huu, Wairani waliojisajili watahiji mwakani. Idadi ya Wairani wanaotazamiwa kutekeleza Hija mwaka  huu ni 87,550.

Siku chache zilizopita, Waziri wa Hija wa Saudi Arabia amewataka Waislamu kote duniani kusitiha kwa muda maandalizi ya ibada ya mwaka huu ya Hija hadi pale hali ya mambo kuhusiana na maambukizi ya virusi vya corona duniani itakapobainika vyema.

Waziri wa Hija wa Saudi Arabia ,Mohammed Saleh Benten amesema, katika mahojiano na televisheni amesema, kwa kuzingatia hali ya sasa ya janga la ugonjwa wa COVID-19 au corona na kwa kutilia maanani kuwa suala la afya ya mahujaji linapewa umuhimu; Saudia inawaomba Waislamu katika nchi zote kusubiri kabla ya kufanya maandalizi ya Hija hadi pale hali itakapoboreka.

Tarehe 18 mwezi uliopita wa Machi Saudi Araba ilipiga marufuku ibada ya Swala katika misikiti miwili mitakatifu zaidi ya Makka na Madina kwa hofu ya maambukizi ya virusi vya corona na imesimamisha ibada ya Umrah kwa Waislamu wote.

Zaidi ya watu 2,752 wameambukizwa virusi vya corona nchini Saudi Arabia na 38 miongoni mwao wameripotiwa kufariki dunia.

3889796

captcha