IQNA

Misikiti Korea Kusini yafunguliwa baada ya kupungua hatari ya corona

19:19 - May 05, 2020
Habari ID: 3472736
TEHRAN (IQNA) – Waislamu Korea Kusini wameamua kufungua misikiti yao Jumatano baada ya nchi hiyo kutoripoti maambukizi mapya ya corona au COVID-19 kwa siku ya tatu mfululizo.

Jumuiya ya Waislamu wa Korea imesema misikiiti hiyo kwa sasa itafunguliwa kwa ajili ya swala za Ijumaa na swala za Tarawih katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Jumuiya hiyo imewataka Waislamu nchini humo kufuata taratibu zilizowekwa na serikali  ili kuzuia  kuenea COVID-19 hasa kuzingatia umbali wa mita moja baina ya waumini wakati wa kuswali.

Kufuatia kuibuka ugonjwa wa COVID-19, serikali ya Korea Kusini ilitaka jamii za kidini kupunguza mijumuiko ili kuzuia kuenea ugonjwa huo.

Waislamu wanaofika misikitini Korea Kusini wametakiwa kuvaa maski au barakoa, kusafisha mikono yao kwa sanitaiza  na kujisajili kabla ya kuingia msikitini.

Korea Kusini imeanza kupunguza vizingiti vilivyowekwa ili kuzuia kuenea corona ambapo wanafunzi wataruhusiwa kuenda shuleni na maeneo mengine ya umma yatafunguliwa. Serikali ya Seoul imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti kuenea ugonjwa huo hatari ambao ungali unaenea kwa kasi maeneo mengine duniani.

Hadi kufikia Mei 5, watu 10,804 walikuwa wameabukizwa corona nchini Korea Kusini na miongoni mwa0 9, 283 wameripotiwa kupona huku 245 wakiaga dunia.

3471362

captcha