IQNA

Kamati ya Katiba ya Ureno yatupilia mbali pendekezo la marufuku ya ufadhili wa misikiti

11:15 - November 21, 2025
Habari ID: 3481549
IQNA – Kamati ya Masuala ya Katiba ya Ureno imeamua kuwa pendekezo la kuzuia ufadhili wa umma kwa ujenzi wa misikiti halina msingi wa kikatiba.

Alhamisi, kamati hiyo ilitoa uamuzi wake wakati wa kupitia marekebisho yaliyopendekezwa na chama cha Chega katika bajeti ya taifa ya mwaka 2026. Marekebisho hayo yalilenga kuzuia fedha za serikali kutumika kujenga misikiti.

Kikao kilifanyika asubuhi ya majadiliano ya bajeti, ambapo kamati ilikubali maoni yaliyoandaliwa na Francisco José Martins wa Chama cha Kidemokrasia cha Kijamii (PSD), kwa mujibu wa The Portugal News.

Hati hiyo ilihitimisha kuwa marekebisho hayo hayalingani na Katiba ya Ureno.

Wajumbe wa Chama cha Kisoshalisti (PS), PSD, Chama cha Kikomunisti cha Ureno (PCP), Livre na Chama cha Watu (JPP) waliunga mkono maoni hayo. Chega walipinga, huku CDS-PP wakijizuia kupiga kura.

Maoni ya kamati yalieleza kuwa pendekezo hilo ni “ubaguzi wa wazi kwa misingi ya dini” na linazua “ubaguzi wa kiholela na usio na mantiki katika haki ya kutendewa sawa.”

Aidha, kamati iliongeza kuwa hatua kama hizo zinakiuka dhamana za kikatiba za usawa na uhuru wa kidini.

Ureno inatambua rasmi Uislamu kama mojawapo ya dini zilizosajiliwa nchini humo. Waislamu nchini Ureno wanakadiriwa kufikia kati ya 60,000–65,000, sawa na takriban 0.6% ya idadi ya watu.

Idadi kubwa ya Waislamu hao wanaishi Lisbon, huku jamii ndogo zikiwa Porto, Faro na Madeira.

3495473

Kishikizo: ureno misikiti waislamu
captcha