IQNA

Nasrallah: Marekani inapanga njama dhidi ya Lebanon

21:47 - June 17, 2020
Habari ID: 3472874
TEHRAN (IQNA) - Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa machafuko yanayoshuhudiwa sasa nchini humo ni njama iliyopangwa na Marekani.

Akizungumza Jumanne usiku kwa njia ya Televisheni, Sayyid Hassan Nasrallah amesema ghasia na machafuko ya sasa ambayo yamepelekea kujeruhiwa makumi ya watu ni njama iliyopangwa na Marekani na inatekelezwa na mirengo ya ndani ya Lebanon.

Sayyid Nasrallah amesisitiza, Marekani ndiyo sababu kuu ya kuadimika fedha za kigeni nchini Lebanon na kupungua thamani ya fedha ya nchi hiyo. Katibu Mkuu wa Hizbullah anasema: "Serikali ya Marekani inazuia kuingizwa sarafu ya dola nchini Lebanon na inaishinikiza Benki Kuu ya nchi hii kwa kisingizio kwamba, fedha za dola zinazokusanywa Lebanon zinapelekewa Syria." 

Sayyid Nasrallah aliongeza kuwa: "Mgogoro wa sasa katika soko la fedha za kigeni nchini Lebanon ni njama iliyopangwa na Marekani na Mkuu wa Benki Kuu Riad Salamé anapaswa kuulizwa kwamba, fedha zimekwenda wapi na zimetoka vipi nje ya nchi?"

Katika hotuba yake, Sayyid Nasrallah amegusia kadhia ya silaha za Hizbullah na kusema: "Silaha za Hizbullah katika mazingira ya Lebanon ni sehemu ya utamaduni na suala la kistratijia ambalo limekita mizizi kiasi kwamba halipaswi kujadiliwa na yeyote."

Katibu Mkuu wa Hizbullah pia ameashiria namna  wanaoshiriki katika maandamano ya sasa nchini Lebanon walivyojikita zaidi katika kutoa nara na uvumi dhidi ya harakati ya Hizbullah na kusema nara uvumi huo unatayarishwa ndani ya jengo la ubalozi wa Marekani mjini Beirut. Miongoni mwa nara na uvumi unaosambazwa ni pamoja na ule unaotoa wito wa kujiuzulu serikali ya Waziri Mkuu wa sasa wa nchi hiyo Hassan Diab. Sayyid Nasrullah anasema: "Maslahi ya Lebanon yamo katika kuendelea kuwepo madarakani serikali ya sasa ili iendeleze juhudi za kufanya marekebisho."

 

3471728/

captcha