IQNA

Mauaji ya Waislamu Srebrenica yalijiri kutokana na EU na UN kutotekeleza majukumu yao

12:13 - July 12, 2020
Habari ID: 3472955
TEHRAN (IQNA) - Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mauaji ya kimbari ya maelfu ya Waislamu wa Srebrenica yalifanyika kutokana na Ulaya kufeli kutekeleza majukumu yake ya msingi.

Mohammad Javad Zarif amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, kwa mnasaba wa kumbukumbu ya miaka 25 tangu yalipotokea mauaji hayo ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Bosnia Herzegovina.

Zarif amesema, "miaka 25 iliyopita, mauaji ya kimbari ya Srebrenica yalianza huku Ulaya ikishindwa kutekeleza wajibu wake wa msingi. Zaidi ya robo karne baadaye, Ulaya ingali imegubikwa na udhaifu huo."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza bayana kuwa, kushindwa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua yoyote wakati huo, daima kutaiponza taasisi hiyo ya kimataifa, na hilo linapaswa kubakia funzo hadi leo hii.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Jenerali Ratko Mladic, aliyekuwa kamanda wa kijeshi wa Serbia na ambaye aliongoza mauaji hayo ya Waislamu 8,000 wa Bosnia alihukumiwa maisha jela Novemba 2017, miaka 20 baada ya mauaji hayo ya kimbari.

Itakumbukwa kuwa, miaka 25 iliyopita katika siku kama ya jana, Waislamu zaidi ya elfu nane wa mji wa Srebrenica mashariki mwa Bosnia Herzegovina waliuawa kwa umati.

Mauaji hayo yalifanywa na Waserbia wenye misimamo mikali. Maafa hayo yalikuwa mauaji makubwa zaidi ya halaiki kuwahi kutokea barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Wakati wa mauaji hayo ya kimbari, wanajeshi wa kulinda amani wa Uholanzi waliokuweko katika eneo hilo hawakuchukua hatua yoyote ya kuwahami Waislamu hao wa Srebrenica. 

3471965

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha