IQNA

Iran yalaani vikali uanzishwaji uhusiano wa kidiplomasia baina ya Bahrain na Israel

19:07 - September 12, 2020
Habari ID: 3473162
TEHRAN (IQNA) - Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekosoa hatua ya kuanzishwa uhusiano rasmi wa kidiplomasia kati ya Bahrain na utawala haramu wa Israel na kusisitiza kuwa, kitendo hicho ni cha fedheha na kudhalilisha.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu imebainisha kuwa, hatua ya Bahrain ya kuufanya wa kawaida uhusiano wake na utawala pandikizi wa Israel inaenda kinyume kabisa na kilio cha wananchi wa Palestina.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa: Kitendo hiki cha aibu na idhilali kilichofanywa na Bahrain, 'kimechinja' azma na ndoto ya miongo kadhaa ya Wapalestina na kupuuza matatizo yao. Hatua hii imechukuliwa kwa maslahi ya uchaguzi mkuu wa Marekani na kwa madhara ya wananchi wa Palestina.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa, kwa hatua yao hiyo, watawala wa Bahrain sasa ni washiriki wa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ni tishio la kudumu la usalama katika eneo la Asia Magharibi na ulimwengu wa Kiislamu. Taarifa hiyo imekumbusha kuwa, utawala haramu wa Israel ndilo chimbuko la ghasia, mauaji, mizozo, ugaidi, na umwagaji damu huko Palestina na katika eneo zima kwa ujumla.

Rais Donald Trump wa Marekani usiku wa kuamkia leo alitangaza kuwa Bahrain na Israel zimefikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina yao, mwezi mmoja baada ya Umoja wa Falme za Kiarabu kuchukua hatua kama hii. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetahadharisha kuwa, utawala wa Manama unapaswa kuwa tayari kubeba dhima ya chochote kitakachofanyika kufuatia uamuzi wake huo wa kuukumbatia hadharani utawala wa Kizayuni.

3922330

Kishikizo: israel bahrain iran
captcha