IQNA

Ayatullah Sheikh Isa Qassim

Uhusiano na utawala wa Israel ni kinyume cha matakwa ya mataifa ya Waarabu

20:15 - September 13, 2020
Habari ID: 3473165
TEHRAN (IQNA)- Mwanazuoni wa ngazi za juu nchini Bahrain Ayatullah Sheikh Isa Qassim amesema kuanzisha uhusiano wa kawaida na kati ya nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kinyume cha matakwa ya wananchi katika nchi hizo.

Katika taarifa , Sheikh Qassim ametoa wito kwa wananchi wa eneo kupinga hatua ya tawala za nchi zao kuanzisha uhusiano na utawala bandia wa Israel. Amesema mapatano yaliyofikiwa hivi karibuni baina ya Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain ni kinyume cha matakwa ya wananchi.

Huku hayo yakijiri, Wananchi wa Bahrain leo wamejitokeza kwa wingi katika maandamano ya kupinga hatua ya utawala wa nchi hiyo ya kufikia makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel.

Maandamano hayo yamefanyika licha ya vikosi vya usalama kupelekwa katika mitaa mbalimbali ya mji mkuu Manamana ili kuzuia maandamano hayo.

Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu walisikika wakipiga nara za kupinga makubaliano ya utawala wa Kifalme wa nchi hiyo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala vamizi wa Israel.

Aidha waandamanaji hao wamepiga nara za "Mauti kwa Marekani na Mauti kwa Israel na kuzikanyagakanyaga bendera za Marekani na Israel.

Mapema  Ijumaa, 12 Septemba, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa Bahrain na Israel zimefikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina yao.

Ikumbukwe kuwa utawala wa Bahrain umechukua hatua ya kusaliti malengo matukufu ya Palestina na Ulimwengu wa Kiislamu kwa kuamua kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, ukiwa umepita mwezi mmoja tu tangu Umoja wa Falme za Kiarabu nao pia kuchukua hatua kama hiyo ambayo imekosolewa vikali na kulaaniwa na  makundi ya Palestina, nchi za Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi na shakhsia kadhaa wa kisiasa, kijamii na kidini kote duniani.

Rais wa Marekani, Donald Trump amekuwa akifanya njama za kila namna za kuhakikisha nchi za Kiarabu zinakuwa na uhusiano wa kawaida na utawala pandikizi wa Israel. Siku ya Alkhamisi ya tarehe 13 Agosti, Umoja wa Falme za Kiarabu  na utawala wa Kizayuni zilifikia makubaliano ya kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia baina yao.

3472547

captcha