IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Hotuba ya Miladj un Nabii SAW

Sera za Iran kuhusu Marekani hazibadiliki kwa kuondoka na kuja rais mwingine

16:24 - November 03, 2020
Habari ID: 3473323
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia siasa za kimantiki za kusimama kidete kukabiiliana na sera za kibabe za Marekani na kusema kuwa, sera zenye mahesabu za Jamhuri ya Kiislamu hazibadiliki kwa kuondoka kiongozi na kuja mwingine madarakani huko Marekani.

Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo mjini Tehran katika hotuba iliyorushwa hewani katika televisheni ya taifa akiupongeza Umma wa Kiislamu kwa mnasaba wa Maulidi na sikukuu ya kuzaliwa Mtume Muhammad SAW na mjukuu wake, Imam Jaafar Swadiq AS.

Amesema kuwa, hali ya sasa ya Marekani inavutia macho na mazingatio ya walimwengu na kuongeza kuwa: Rais wa jamhuri ambaye anashika madaraka ya nchi kwa sasa na ambaye ndiye anayesimamia zoezi la uchaguzi anasema uchaguzi huo ndio utakaokuwa na uchakachuaji mkubwa zaidi katika historia ya Marekani; huku mpinzani wake akisema Trump ana nia ya kufanya udanganifu katika uchaguzi.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa hali hii ni mfano wa sura ya kuchukiza ya demokrasia ya kiliberali na kuongeza kuwa, bila ya kujali nani atashinda uchaguzi wa Marekani, hali ya sasa ya nchi hiyo inaakisi kuporomoka sana kijamii, kisiasa na kimaadili nchini Marekani, na hatima ya mfumo kama huu wa kisiasa ni kunyauka na kusambaratika. 

Ayatullah Khamenei amesema kuwa sababu kuu ya uadui wa Marekani dhidi ya utawala wa Kiislamu nchini Iran ni msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu wa kupinga sera za kidhalimu na kukataa kutambua rasmi ubeberu wao. Amesema kuwa, uadui huo utaendelea, na njia pekee ya kukabiliana nao ni kuwavunja moyo wale wanaodhani kwamba wanaweza kutoa pigo kubwa kwa taifa na serikali ya Iran. 

Hasira ya Waislamu kuhusu kuvunjiwa heshima Mtume SAW ni ishara ya uhai wa umma

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa hasira na malalamiko ya Waislamu kote duniani dhidi ya vitendo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW ni ishara ya kuwa hai Umma wa Kiislamu.

Ayatullah Khamenei ameashiria vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume (saw) nchini Ufaransa na kusema kuwa: Mchora vibonzo mmoja amefanya makosa katika tukio hilo, lakini huu si upofu na uovu wa msanii mmoja, bali ni siasa za serikali ambayo imeunga mkono na kukingia kifua uozo huo, na ni makosa ya kiongozi wa kisiasa ambaye ametetea waziwazi uhalifu huo.

Kiongozi Muadhamu wa Mpinduzi ya Kiislamu amesema kuwa serikali ya Ufaransa imeutaja uozo huo kuwa ni haki ya binadamu na uhuru wa kujieleza, na hii ndiyo siasa ileile inayowapa hifadhi makatili wakubwa zaidi duniani. 

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, serikali ya Ufaransa ilimpa msaada mkubwa zaidi mbwa mwitu na mwagadamu mkubwa mithili ya Saddam Hussein wakati wa vita vya kutwishwa dhidi ya Iran na kuongeza kuwa: Kutetea ukatili wa kiutamaduni na jinai ya mchora vibonzo vinavyomdhalilisha Mtume SAW ni sehemu ya pili ya sarafu moja ya kuwaunga mkono magaidi na Saddam.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, hasira na malalamiko ya Umma wa Kiislamu dhidi ya kitendo hicho cha kumtusi na kumvujia heshima Mtume SAW ni ishara ya kuwa hai Umma wa Kiislamu na kusema, wapo baadhi ya watawala ambao wamedhihirisha tena uduni na udhalili wao katika kadhia hii, lakini aghlabu ya mataifa ya Kiislamu yametetea utambulisho na matukufu yao.

3933049/

captcha