IQNA

Hamas yalaani kauli ya waziri wa Bahrain kuhusu bidhaa zinazozalishwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni

20:06 - December 04, 2020
Habari ID: 3473421
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imelaani kauli aliyotoa waziri wa biashara, viwanda na utalii wa Bahrain kuhusu azma ya nchi yake ya kununua bidhaa zinazozalishwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwenye Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan.

Msemaji wa Hamas Sami Abu Zuhri amesema, matamshi ya waziri wa biashara wa Bahrain kwamba nchi yake itanunua bidhaa zinazozalishwa katika vitongoji hivyo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Abu Zuhri ameongeza kuwa, matamshi ya aina hiyo yanayotolewa na viongozi wa Bahrain yanaonyesha jinsi walivyoporomoka na kuamua kusimama kwenye safu moja na maghasibu dhidi ya Wapalestina.

Msemaji wa Hamas amewataka wananchi wa Bahrain waishinikize serikali yao iachane na kile alichokiita "misimamo ya kidhalili na ya kuipiga vita Palestina".

Waziri wa biashara, viwanda na utalii wa Bahrain Zayd bin Rashid Az-Zayani amesema, nchi yake haitafautishi kati ya bidhaa zinazozalishwa na Israel na zile zinazotoka kwenye vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ufukwe wa Magharibi na kwa hivyo itazinunua bidhaa hizo pia kwa sababu zote ni za Israel.

Az- Zayani alitoa matamshi hayo siku ya Jumanne katika mazungumzo na viongozi wa utawala haramu wa Kizayuni.

Itakumbukwa kuwa,  katika hatua inayopingana kikamilifu na malengo matukufu ya watu wa Wapalestina ya ukombozi wa nchi yao, tarehe 25 Septemba, mawaziri wa mambo ya nje wa Imarati na Bahrain walisaini mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House mjini Washington na kuhudhuriwa na rais wa Marekani Donald Trump na Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala haramu wa Israel.

3938958

captcha