IQNA

Morocco yakosolewa vikali kwa kuanzisha uhusiano na utawala wa Israel

11:17 - December 11, 2020
Habari ID: 3473444
TEHRAN (IQNA) - Harakati za kupigania ukombozi wa Palestina zimelaani vikali hatua ya Morocco kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na Harakati ya Jihad Islami zimetoa taarifa ambapo zimelaani hatua ya Morocco kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na kuutaja uamuzi huo kuwa ni usaliti kwa mkakati kuikomboa Palestina.

Harakati ya Jihad Islami imesema, 'tunaamini kuwa watu wa Morocco watapinga vikali uamuzi huo wa kuanzisha uhusiano na Israel."

Naye msemaji wa Hamas Hazem Qassem ameutaja uamuzi wa Morocco kuwa ni dhambi.

Kwa upande wake, Bassam As-Salhi, mwanachama wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina amelaani uamuzi huo wa Morocco. Amesema haikubaliki kwa nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano na utawala wa Israel ambao unakalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Jana Alhamisi, Mfalme wa Morocco Mohammed VI alimwarifu rais Donald Trump wa Marekani kwenye mazungumzo kwa njia ya simu kuwa amekubali kurejesha mawasiliano ya kiserikali na kuanzisha uhusiano wa kibalozi na utawala wa Israel haraka iwezekanavyo.

Marekani nayo imesema itatambua mamlaka ya Morocco katika eneo la Sahara Magharibi la nchi hiyo ambalo limejitangazia uhuru. 

Wakati huo huo, Harakati za kupigania ukombozi wa Palestina zimelaani vikali hatua ya Morocco kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Harakati ya Ansarullah ya Yemen imelaani hatua ya ufalme wa Morocco kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika taarifa, msemaji wa Ansarullah Mohammed Abdul Salam amesema hakuna chochote kinachoweza kuhalalisha kitendo cha Morocco kuanzisha uhusiano na adui Mzayuni. Katika taarifa kupitia ukurasa wake wa Twitter, amesema: "Hatua ya nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni inalaaniwa na inapingwa vikali. Serikali yoyote inayodai kuwa ni ya Kiarabu au Kiislamu, haina mmsingi wowote wa kutetea uamuzi wa kuanzisha uhusiano na adui Mzayuni.

Aidha amesema utawala wa Saudi Arabia, ambao unachochoea nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano na Israel, uko mbali sana na masuala muhimu ya umma wa Kiislamu.

Itakumbukwa kuwa, katika hatua inayopingana kikamilifu na malengo matukufu ya watu wa Wapalestina ya ukombozi wa nchi yao, tarehe 25 Septemba, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain walisaini mkataba wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House mjini Washington na kuhudhuriwa na rais wa Marekani Donald Trump na waziri mkuu wa utawala haramu wa Israel Benjamin Netanyahu. Sudan na sasa Morocco pia zimefuata mkumbo huo na kutangaza utayarifu wa kuanzisha uhusiano na utawala huo bandia.

Hatua hizo za nchi za Kiarabu zinaendelea kukosolewa na kulaaniwa vikali na viongozi wa Palestina pamoja na wapenda haki kote duniani wakisema kuwa ni usaliti wa wazi kwa harakati za kupigania ukombozi wa Palestina.

3940369

captcha