IQNA

15:16 - December 12, 2020
Habari ID: 3473449
TEHRAN (IQNA)- Leo Waislamu wa Nigeria wanakumbuka mauaji yaliyotekelezwa na jeshi la nchi hiyo katika mji wa Zaria jimboni Kaduna, dhidi ya wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Katika shambulio hilo la Disemba 12, 2015, inakadiriwa wanachama zaidi ya 1,000 wa harakati ya Kiislamu ya Nigeria, aghalabu wakiwa ni Waislamu wa madhehebu ya Shia waliuawa kwa kufyatuliwa risasi na jeshi la Nigeria. Miongoni mwa waliouawa walikuwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Ibrahim Zakzaky Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Katika siku iliyofuata, Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe Malama Zeenat walitiwa nguvuni wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Hussainia ya Baqiyatullah na nyumba ya mwanazuoni huyo katika mji wa Zaria.

Hatua kandamizi na za kikatili za polisi na jeshi la Nigeria dhidi ya wafuasi wa Sheikh Zakzaky zingali zinaendelea na hadi sasa idadi kubwa ya wafuasi wa kiongozi huyo wa kidini wamewekwa kizuizini au wameuawa shahidi.

Uvamizi huo ulijiri baada ya Jeshi la Nigeria kudai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walikuwa na njama ya kutaka kumuua mkuu wa jeshi hilo, madai ambayo yalikanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo.

Wanaharakati katika maeneo mbali mbali duniani wanaendelea kushinikiza uchunguzi ufanyike kuhusu mauaji ya Zaria. Aidha nchini Nigeria maandamano ya amani hufanyika mara kwa mara ambapo waandamanaji hutangaza kufungamana kwao na Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye anashikiliwa kinyume cha sheria nchini humo. Aidha maandamano ya wananchi wa Nigeria yanaendelea ili kushinikiza kuachiliwa huru mwanaharakati huyo wa Kiislamu ambaye ni mtetezi wa wanaodhulumiwa.

3473366

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: