IQNA

Maandamano makubwa Nigeria ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru

12:01 - October 07, 2020
Habari ID: 3473239
TEHRAN (IQNA) – Mamia ya Waislamu wa Nigeria wameandamana Abuja wakitaka serikali imuachilie huru Kiongozi wa Haraakti ya Kiislamu, Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Maandamano hayo yamefanyika huku kukiwa na mvua kali katika mji huo mkuu wa Nigeria.

Washiriki wamemtaka rais wa nchi hiyo Muhammadu Buhari aamuru kuachiliwa huru mara moja kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) Shekh Zakzaky na mke wake ambao hali zao za kiafya zinazidi kuwa mbaya.

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe Malama Zeenat walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Hussainia ya Baqiyatullah na nyumba ya mwanazuoni huyo katika mji wa Zaria. Waislamu wasiopungua 1,000, wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi katika shambulio hilo.

Mahakama Kuu ya Nigeria iliwahi kutoa hukumu iliyosisitiza kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe hawana hatia yoyote na ikaamuru waachiliwe huru, lakini wawili hao wangali wanaendelea kuwekwa jela na hivi sasa hali zao za afya ni mbaya sana

Wakati huo huo, hatua kandamizi na za kikatili za polisi na jeshi la Nigeria dhidi ya wafuasi wa Sheikh Zakzaky zingali zinaendelea na hadi sasa idadi kubwa ya wafuasi wa kiongozi huyo wa kidini wamewekwa kizuizini au wameuawa shahidi. Aidha vyombo vya usalama vimekuwa vikifanya kkila viwezalo kukwanmisha shughuli za kidini za Waislamu wa Kishia nchini Nigeria.

3927817

Kishikizo: zakzaky nigeria buhari
captcha