Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, mamia ya Waislamu Nigeria wameandamana wakiwa wamebeba mabango katika barabara kuu za Lagos ambapo wamelaani kudhulumiwa wanawake wanaovaa Hijabu.
Mabango hayo yalikuwa na maandishi kama vile "Hijabu Yangu, Heshima Yangu, Chaguo Langu", "Mimi Naipenda Hijabu", "Hijabu na Mapenzi" na "Mimi Ninafuraha kuwa Nina Hijabu".
Hafswa Badru Mkuu wa Jumuiya ya Wanachuo Waislamu Nigeria ameshiriki katika maandamano hayo na kubainisha kutofurahishwa kwake na ongezeko la uvunjiwaji haki wanawake wanaovaa Hijabu.
Amesema kuwa, pamoja na kuwepo upashaji habari kuhusu umuhimu wa Hijabu, bado baadhi ya watu wa Nigeria wanawabughudhu wanawake Waislamu wanaovaa Hijabu. Aidha amelaani jinai za kundi la kigaidi la Boko Haram na kusema wanawake Waislamu kuvaa Hijabu hakumaanishi kuwa wanaunga mkono ugaidi wa Boko Haram.
Hivi karibuni, baada ya kupuuza mauaji yaliyofanywa na jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu katika mji wa Zaria, Rais Muhammadu Buhari alisema iwapo italazimu atapiga marufuku vazi la mwanamke wa Kiislamu la hijabu.
Rais Muhammad Buhari aliyasema hayo jana na kuongeza kuwa, serikali yake haina njia nyingine ghairi ya kuchagua moja kati ya mambo mawili ama vazi la hijabu au usalama na kwamba yeye atalipiga marufuku vazi hilo la staha la mwanamke wa Kiislamu nchini Nigeria.
Jumuiya ya Haki za Waislamu Nigeria ilitoa taarifa na kulaani vikali mpango huo wa Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo kutaka kupiga marufuku vazi la Hijabu.
Jumuiya ya Haki za Binadamu Nigeria mbali na kulaani pendekezo hilo la Rais Buhari ilisema sera kama hiyo ni njia ya kukwepa utatuzi wa matatizo ya kimsingi ya nchi hiyo.