IQNA

22:47 - April 13, 2021
News ID: 3473811
TEHRAN (IQNA) - Kwa mara nyingine tena mbingu zimefunguka na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani uko nasi.

Fungueni nyoyo zenu kwani Ramadhani na baraka zake zote pamoja na uzuri wake imewadia.
Ramadhani sawa na huko nyuma kwa usahali na bila ria lakini kwa kina na wingi wa maana imewadia ili nyoyo zetu zilizochoka zinufaike na chemichemi yake na rehma za Mwenyezi Mungu zitushukie.
Mwezi wa Ramadhani unatoa bishara njema kwa Waisalmu wote kuhusu kufunguliwa milango ya peponi na kuanza karamu ya Mwenyezi Mungu.

Fursa nzuri

Kwa hakika Mwenyezi Mungu ametuita ili tuweze kunufaika vya kutosha na chemichemi hii yenye neema zake kubwa. Hakuna shaka kuwa mwanaadamu anahitaji kutumia vizuri fursa iliyojitokeza katika Mwezi wa Ramadhani ili anong'one na Mola wake.
Mwezi wa Ramadhani umewadia baada ya kupita siku zilizojaa misukosuko ili kuweza kutupatia utulivu wa kweli. Iwapo tutautambua Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa hazina isiyo na kifani na kuzingatia lahadha zake zenye thamani, basi hakuna shaka kuwa mazingira mapya yataibuka katika maisha yetu. Katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani Mwenyezi Mungu anawapa fursa waja wake ili kwa mara nyingine tena waweze kuchunguza upya maisha yao na kuondoa mzigo mzito wa madhambi.

Nyakati safi na takatifu


Mwenyezi Mungu ameufanya Mwezi huu kuwa na nyakati safi na takatifu kwa ajili ya mja kuomba dua, toba na kujikurubisha kwa Muumba wake. Mwezi wa Ramadhani ni wakati ambao madhambi na mabaya huchomeka na amali njema kuongezeka maradufu.
Ramadhani ni msafiri tunayemjua ambaye akiwa na shanta linalobeba bishara njema huchukua njia ya kutoka mbinguni hadi vichochoro vya ardhini na kusambaza mizigo yake.
Salamu ziwe kwako ewe Mwezi wa Mwenyezi Mungu! Salia na watu wa dunia, leta utulivu katika nyakati zetu, bakia pembeni mwetu. Salamu ziwe kwako ewe dhihirisho la mapenzi ya Mwenyezi Mungu! Ewe mwenezaji wa rehemu za Mwenyezi Mungu! Kuja kwako kunaashiria mwanaadamu kufikia kilelele cha ucha Mungu.
Tutendeni amali njema na tuondoe vumbi la kughafilika kutoka katika nyoyo zetu. Mwenyezi Mungu Karimu anatusubiri ili tuweze kufika chini ya kivuli cha neema na mapenzi yake. Tunufaike na nyakati tamu za ucha Mungu katika mwezi huu.

Taufiki ya kufunga


Ewe Mola Muumba! Tunakushukuru kwa ajili ya kutupa uhai na kutuwezesha kwa mara nyingine kuona nuru ya kuvutia ya hilali ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Yarabi! Tupe taufiki ili tuweze kufunga na tuweze kutii amri yako kwa hamu na raghba.
Ewe Mola Muumba! Tunakushukuru kwa kututunuku nyakati hizi zilizojaa nuru. Ewe Mola! Tumefika katika njia hii nyoofu ili jangwa la nyoyo zetu ziweze kupata neema ya mvua yako na kubadilika kuwa bustani la mapenzi na imani. Ya Rabi! Tumekuja mbele yako kwani hakuna yeyote anayestahiki nyoyo zetu isipokuwa Wewe tu. Tunafungua madirisha ya nyoyo zetu ili upepo mwanana wa kukukumbuka uweze kututuliza.
Ya Rabi! Tunanyoosha mikono yetu mbele yako ili kwa ukarimu wako ukidhi mahitaji yetu na uweze kutukubali katika mankuli ya mbinguni katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Bishara njema

Katika masaa ya awali ya mwezi huu azizi tusikilize maneno ya Mtume Mtukufu wa Uislamu Mohammad SAW. Alitoa bishara zifuatazo kufuatia kuwadia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani:
"Enyi Watu, Mwezi wa Mwenyezi Mungu wenye baraka, rehema na maghfira umewadia mbele yenu. Mwezi ambao mbele ya Mwenyezi Mungu ndio mwezi bora zaidi na siku zake ni ndizo siku bora zaidi na masaa yake ndiyo masaa bora zaidi. Mwezi ambao ndani yake mnaalikwa kuwa wageni wa Mwenyezi Mungu. Amali zenu katika mwezi huu zinakubalika na dua zenu zinajibiwa. Basi kwa nia safi na nyoyo zilizotakasika, muombeni Mola wenu awape taufiki ya kufunga na kusoma Quran katika Mwezi huu.

Kuwasaidia wasiojiweza

Katika mwezi huu wasaidieni masikini, heshimuni wazee na waonyesheni ukarimu watoto na tembeleeni jamaa zenu. Zuia ulimi kuzungumza maneneo yasiyofaa. Epusheni macho yenu kutazama vitu visivyofaa na haramu. Zuieni masikio kusikia mambo yasiyofaa....Enyi watu! Kila ambaye akhlaqi zake zitakuwa nzuri katika Mwezi huu, siku ambayo miguu itatetemeka katika daraja la serat, atapita hapo kwa njia sahali. Kila ambaye katika mwezi huu atawatembelea jamaa, Mwenyezi Mungu atamarehemu katika siku ya Qiyama.... Katika nyakati za swala inueni mikono yenu kwa ajili ya dua. Hii ni kwa sababu wakati wa swala ndio wakati bora zaidi na wakati huo, Mola huwatizama waja kwa jicho la rehema. Iwapo mtamuomba basi atawajibu.

Milango ya pepo iko wazi


Enyi watu! Katika mwezi huu milango ya pepo iko wazi, muombeni Mola wenu asiwafungie milango hii. Milango ya jahanam katika mwezi huu imefungwa. Muombeni Mwenyezi Mungu asiwafungulie milango hiyo."

Imam Swadiq AS anasema: "Siku moja Mwenyezi Mungu alimshushia Wahyi Nabii Dawud na kumwambia, ‘nenda kwa mwanamke aiitwaye Halaw na umpe bishara ya zawadi ya pepo na kisha mwambie kuwa mtakuwa pamoja. Dawud alienda nyumbani kwa mwanamke huyo na akabisha mlango. Mwanamke akatoka nje ya nyumba na alipomwona Mtukufu huyo akasema: "Ewe Daud Nabii! Ni nini kimefanya uje hadi nyumbani kwangu"?. Daud A.S. akasema: "Ewe mwanamke! Umenishukia wahyi kutoka kwa Haki kuhusu fadhila zako." Mwanamke huyo huku akiwa amestaajabu akasema: "Pengine mwanamke huyo si mimi. Yamkini anashabihiana nami. Naapa kwa Mola kuwa hakuna kazi ambayo nimefanya ili niweze kufikia daraja kama hii". Nabii Daud akasema: "Mwanamke huyo ni wewe. Hebu nifahamishe kidogo kuhusu maisha yako." Mwanamke akasema: "Ewe Daud Nabi! Mimi nimepata masaibu na mashaka mengi katika maisha yangu. Kila machungu na matatizo yanaponipata maishani, husubiri na kwa kumshukuru Mola, huishi na matatizo hayo. Sikumbuki kumuomba Mwenyezi Mungu aniondolee matatizo bali mimi humuomba tu anipe nguvu ya kuvumilia matatizo na mashaka." Nabii Daud katika kumjibu mwanamke huyo akasema: "Ni kwa sababu hii- ya kuwa na subira na kuridhia- ndio umeweza kufika katika daraja hii."

Faradhi


Hivi sasa nwezi wa Ramadhani, mwezi wa saumu uko nasi. Kwa mujibu wa amri ya Mwenyezi Mungu SWT tunapaswa kufunga kwa muda mwezi mmoja. Ibada hii ni faradhi.
Katika Suratul Baqara Aya ya 187 Mwenyezi Mungu SWT anasema: "Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni saumu mpaka usiku."
Kujiepusha kula na kunywa ndilo sharti la kwanza la saumu. Lakini je saumu ni kuzuia kula na kunywa tu?
Iwapo mtu aliye katika saumu hatahifadhi viungo vya mwili wake kutofanya madhambi. Basi saumu itakuwa haina faida ila mashaka ya njaa na hivyo moyo wa mwanaadamu hautaweza kunufaika na uzuri na utukufu wa mwezi wa Ramadhani. Wakati mwanaadamu mwenye kufunga anapoanza saumu yake basi wakati huo nguvu ya subira yake mbele ya dhambi na maasi huongezeka. Hatua kwa hatua moyo hubadilika na athari hiyo kudumu moyoni mwake.
Mja anayefunga wakati shetani anampomshawishi hujifunza namna ya kuimarisha taqwa yake kwa msaada wa Mwenyezi Mungu.
Imam Swadiq AS anasema: "Njaa ni nuru ya moyo wa Muumini."
Hii ina maana kuwa kustahamili njaa na kujizuia na matamanio ya nafsi ni njia muafaka ya kustawisha moyo na kujenga uwezo halisi wa mwanaadamu.

Wageni wa Mwenyezi Mungu

Iwapo mwanaadamu atatumia uwezo wake wote katika njia ya matakwa na matamanio yake ya kimwili, huwa hakuna tena fursa inayobakia ya kukuza umaanawi.
Kwa hivyo tunaweza kufikia natija hii kuwa saumu ina falsafa ya juu zaidi ambayo ni kuandaa mazingira ya kukuza moyo na nafsi ili mwanaadamu aweze kuondoka katika gereza la mwili na kuchukua mkondo wa ukamilifu.
Imam Baqir AS anasema: "Ramadhani ni Mwezi wa Mwenyezi Mungu na wanaofunga katika mwezi huu ni wageni wa Mwenyezi Mungu na wanapewa heshima maalumu."

Tags: ramadhani ، mwezi
Name:
Email:
* Comment:
* captcha: