IQNA

Wagombea urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wabainika

19:30 - May 25, 2021
Habari ID: 3473945
TEHRAN (IQNA) - Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetaja majina ya wagombea wa urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao wa Juni humu nchini.

Katika taarifa yake ya leo Jumanne, tume ya uchaguzi ya Iran imetangaza majina ya wagombea katika uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliotimiza masharti ya kugombea kwa mujibu wa sheria za uchaguzi za Jamhuri ya Kiislamu.

Taarifa hiyo imesema, katika utekelezaji wa kifungu cha 60 cha sheria ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu, majina ya wagombea wa uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliotimiza masharti na kupasishwa na Baraza la Kulinda Katiba ni kama ifuatavyo:

Saeed Jalili, Mohsen Rezaee Mirgha'ed, Sayyid Ebrahim Raisol-Sadati (Ebrahim Raisi), Alireza Zakani, Sayyid Amir-Hossein Ghazizadeh Hashemi, Mohsen Mehralizadeh na Abdolnaser Hemmati.Wagombea urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wabainika

Jumla ya watu 592 walikuwa wamewasilisha majina yao wakitaka kuidhinishwa wagombee urais ambapo majina hayo yamechujwa na Baraza la Kulinda Katiba, ambalo lina jukumu la kisheria kusimamia uchaguzi na kuwachunguza wanaotaka kugombea kabla ya kuwaidhinisha.

Baraza hilo limesema miongoni mwa watu hao 592, ni 40 pekee waliowasilisha nyaraka zote zinazohitakija na miongoni mwao 7 ndio waliotimiza vigezo vya kisheria vya kuwa wagombea urais.

Kwa mujibu wa kifungu cha 66 cha sheria, kampeni za uchaguzi za wagombea wa urais zinaanza rasmi siku na tarehe ya kutangazwa majina ya wagombea na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran. Kampeni hizo zinaendelea hadi masaa 24 kabla ya kuanza zoezi la kupiga kura.

Wagombea wote nchini Iran wanapewa haki sawa kwa kuhesabiwa mpaka sekunde za kufanya kampeni katika vyombo vya habari vya taifa kama vile redio na televisheni, bila ya kupunguziwa au kuongezewa hata sekunde moja.

Uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uchaguzi wa 6 wa mabaraza ya Kiislamu ya miji na vijiji unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya tarehe  18 mwezi ujao wa Juni, 2021.

3973704

captcha