IQNA

Rais wa Afghanistan atoroka nchi baada ya Taliban kudhibiti Kabul

20:50 - August 15, 2021
Habari ID: 3474191
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani ameikimbia nchi yake leo jioni baada ya kundi la Taliban kuchukua udhibiti wa mji mkuu wa Kabul. Taarifa zinasema Ghani ameondoka Afghanistan na inaarifiwa amekimbilia taifa jirani la Tajikistan.

Mkuu wa Baraza la Maridhiano ya Taifa nchini Afghanistan Abdullah Abdullah pia amethibitisha habari hizo kupitia mkanda wa video.Kuondoka kwa Ghani kunatoa taswira halisi ya uwezekano wa kundi la Taliban kuchukua madaraka nchini Afghanistan wakati wowote kuanzia sasa.

Wapiganaji wa kundi hilo waliingia kwenye viunga vya pembezoni mwa mji mkuu wa Kabul leo Alfajiri baada ya kupata mafanikio makubwa katika siku za karibuni kwa kuikamata miji mingi nchini humo.

Jumapili ya leo wapiganaji wa Taliban walizingira makao makuu ya utawala wa Afghanistan, Kabul, na kutangaza kuwa wamewaamuru wapiganaji wa kundi hilo kujiepusha na utumiaji wa mabavu na kutoa njia salama kwa mtu yeyote anayetaka kuondoka Kabul.

Wanamgambo wa Taliban wamekaribia kuithibiti nchi nzima ya Afghanistan, huku mji mkuu wa nchi hiyo Kabul ukiwa umedhibitiwa pia na kundi hilo.

Hali ya usalama nchini Afghanistan imezorota katika wiki za hivi karibuni kufuatia uondoaji usio wa kuwajibika wa askari wa Marekani. 

Sambamba na kundi la Taliban kuendelea kuteka maeneo zaidi huko Afghanistan na kuongezeka wasiwasi kuhusu mustakbali wa nchi hiyo, Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza alisema Ijumaa kwamba hali ya Afghanistan ni mbaya mno na kwamba inatokana na uamuzi wa Rais Joe Biden wa kuondoa askari wa Marekani nchini humo.

3475503

 

captcha