IQNA

Iran yatoa wito kwa wanaohusika katika vita Afghanistan kusitisha mapigano

21:01 - August 08, 2021
Habari ID: 3474171
TEHRAN (IQNA)- Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa wito kwa pande zote katika vita nchini Afganistan kusitisha vita na mauaji ya ndugu kwa ndugu sambamba na kufanya mazungumzo ya kutatua mgogoro uliopo huku ikitangaza kuwa tayari kuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo.

Hayo yamo kwenye taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran katika kumbukumbu ya tukio la kigaidi la kuuawa wanadplomasia na mwandishi habari wa Iran katika eneo la Mazar-e-Sharif. Taarifa hiyo imesema: "Agosti nane ni moja ya siku zenye uchungu katika diplomasia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika siku kama hii miaka 23 iliyopita, wanadiplomasia  wa Iran na mwandishi habari waliuawa shahidi katika hujuma iliyotekelezwa dhidi ya Ubalozi Mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Maza-e-Sharif Afghanistan. Hujuma hiyo ilikuwa kinyume cha mikataba yote ya kimataifa, Uislamu na mantiki ya binadamu."

Taarifa hiyo  imesema jamii ya kimataifa ilifungamana na Iran kufuatia hujuma hiyo ya kigaidi na watu wa Afghanistan nao vile vile walijiunga na Iran katika maombolezo kwani wao wenyewe ni wahanga wa ugaidi na nukka hiyo inaashiria uhusiano wa kina baina ya watu wa nchi mbili. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema Iran, sawa na miaka ya nyuma, inasimama pamoja na watu wa Afghanistan na iko tayari kuunga mkono suluhisho lololote lile ambalo litapelekea kumalizika vita vya zaidi ya miongo minne Afghanistan. 

Wakati huo huo, kundi la Taliban nchini Afghanistan limendelea kupambana na jeshi la serikali katika mikoa mitatu ya kaskazini mwa nchi hiyo ya Kunduz, Sar-e-Pul na Jawzjan huku taarifa zikisema raia wameuawa katika mapigano hayo.

Kundi la Taliban limedai leo kwamba limeuteka mji muhimu wa Afghanistan wa Kunduz. Mashirika kadhaa ya habari yamethibitisha kuwa mji wa Kunduz unashikiliwa na wapiganaji wa Taliban na kwamba wamechukua mitambo yote muhimu ya mji huo.

3475453

Kishikizo: iran afghansitan
captcha