IQNA

20:02 - August 16, 2021
Habari ID: 3474196
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anafuatilia hali ilivyo huko Afghanistan akiwa na wasiwasi mkubwa na amewasihi Taliban na wahusika wote wajizuie kwa kiwango cha juu ili kuepusha madhara kwa raia na pia kuhakikisha utoaji wa misaada ya kibinadamu.

“Mzozo huo unalazimisha maelfu ya watu kuondoka katika nyumba zao. Kuna ripoti zinazoendelea za ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika jamii zilizoathiriwa na mapigano.” Imesema taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa na msemaji wake, Stephane Dujarrick mjini New York Marekani Jumapili.  

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, Jumapili hii Wataliban ambao tayari wanadhibiti sehemu kubwa ya Afghanistan, wameingia katika mji mkuu, Kabul, wakati Rais Ashraf Ghani na maafisa wengine wakitoroka nchi.

Katibu Mkuu Guterres ametoa wito kwa Taliban na pande zote kutii kanuni za sheria za kimataifa za kibinadamu, na kulinda na kuheshimu haki na uhuru wa raia wote. 

"Katibu Mkuu ana wasiwasi hasa juu ya mustakabali wa wanawake na wasichana, na haki zao ambazo zilipatikana kwa taabu lazima zilindwe." imesema taarifa hiyo. 

Msemaji wa kundi la Taliban ametaka iundwe serikali ya Kiislamu nchini Afghanista inayoendana na mazingira itakayojumuisha na Waafghani wengine pia.

Suhail Shaheen ameyasema hayo leo katika mji mkuu wa Qatar, Doha na kusisitiza kuwa serikali mpya itakayoundwa nchini Afghanistan haitahusisha wanachama wa kundi hilo peke yao.

Shahen ameongeza kuwa Taliban inataka shakhsia mbalimbali maarufu wa Afghanistan washiriki katika serikali mpya itakayoundwa na kundi hilo.

Halikadhalika msemaji huyo wa Taliban amesema, kundi hilo litawahakikishia usalama wanajeshi na askari wa vikosi vya usalama watakaokabidhi silaha zao na kujiunga na kundi hilo.

Kabla ya tangazo hilo, viongozi wa Taliban waliliambia gazeti la Times la Uingereza kuwa kundi hilo haliafiki wazo la kuundwa serikali ya mpito nchini Afghanistan.

Wapiganaji wa kundi la Taliban, jana Jumapili Agosti 15 waliingia mji mkuu wa Afghanistan, Kabul sambamba na kuanguka kwa serikali kufuatia hatua ya Rais Muhammad Ashraf Ghani kuitoroka nchi.

3991063

Kishikizo: taliban ، afghanistan
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
* captcha: