IQNA

Kiongozi Muadhamu katika ujumbe kufuatia hujuma ya kigaidi msikitini Afghanistan

Wakuu wa Afghanistan wawaadhibu waliouhusika na hujuma dhidi ya msikiti

10:48 - October 10, 2021
Habari ID: 3474404
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ametoa mwito kwa mamlaka za Kabul kuwaadhibu waliohusika na shambulizi la bomu lililoua makumi ya watu msikitini katika mji wa Kunduz nchini Afghanistan juzi Ijumaa.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alitoa mwito huo jana Jumamosi katika salamu za rambirambi kufuatia hujuma hiyo ya kigaidi na kusisitiza kuwa, kuna haja ya kuchukuliwa hatua za kuzuia mashambulio ya aina hiyo kutokea tena.

Kiongozi Muadhamu amesema amesikitishwa mno na tukio hilo lililopelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa idadi kubwa ya watu wasio na hatia nchini Afghanistan., na kuzitaka mamlaka husika nchii humo kuwafikisha mbele ya sheria waliotenda jinai hiyo.

Kadhalika Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mbali na kuwaombea rehema na maghfira waliouawa shahidi katika hujuma hiyo, na kuwatakia majeruhi afueni ya haraka, ameziombea subira na amani familia za wahanga wa shambulio hilo.

Waumini wasiopungua 60 waliripotiwa kuuawa na wengine 150 kujeruhiwa katika mripuko huo  wa bomu uliojiri juzi Ijumaa katika msikiti wa Khan Abad karibu na mji wa Kunduz nchini Afghansitan. Baadhi ya duru zinasema waliouawa shahidi katika hujuma hiyo ni karibu watu 100.

Hujuma hiyo ya kigaidi ilijiri wakati waumini walipokuwa wakiswali Swala ya Ijumaa katika msikiti huo wa Waislamu wa madhehebu ya Shia. Hii ni hujuma ya kwanza kubwa kuwahi kutekelezwa dhidi ya Mashia wa Afghanistan tangu kundi la Taliban lichukue hatamu za uongozi mwezi Agosti. Kundi la kigaidi la ISIS limedai kuhusika na hujuma hiyo ambayo imelaaniwa vikali na viongozi wa Taliban.

4003493

captcha