IQNA

Rais wa Iran atuma salamu za rambi rambi kufuatia kuuawa shahidi waumini msikitini Afghanistan

15:34 - October 09, 2021
Habari ID: 3474400
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma ujumbe kufuatia kuuawa shahidi na kujeruhiwa idadi kubwa ya watu wasio na hatia nchini Afghanistan.

Katika taarifa ya leo Jumamosi, Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma ujumbe na kuashiria hujuma ya kigaidi dhidi ya msikiti wakati wa Swala ya Ijumaa jana katika mji wa Kunduz nchini Afghanistan na kusema: "Jinai ambayo imefanyika kwa lengo la kuibua mifarakano baina ya Waislamu imetekelezwa na watu ambao utambulisho wao ulio dhidi ya ubinadamu na dini uko wazi kwa wote."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kwamba, kuenea  pote la magaidi wakufurishaji kumejiri kwa himaya na kwa mpangilio wa Marekani. Amesema katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imeandaa mazingira ya kustawi na kuenea watenda jinai wa ISIS au Daesh nchini Afghanistan na kwamba ilizuia kuangamizwa kundi hilo la kigaidi.

Rais Ebrahim Raisi katika ujumbe wake amebainisha wasiwasi wake kuhusu kuendelea hujuma za kigaidi pamoja na fitina za kimadhehebu na kikaumu ambazo ni katika njama mpya za Marekani dhidi ya Afghanistan. Aidha amesisitiza kuwa, sawa na miaka ya nyuma, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kuwsaidia na kuwapa himaya wananchi ndugu wa Afghanistan.

Katika ujumbe wake huo, Rais wa Iran ameelezea matumaini yake kwamba, kuwa macho makundi ya Afghanistan sambamba na kuundwa serikali jumuishi kutakuwa na nafasi kubwa katika kusambaratisha njama hizo na hivyo kuwawezesha watu wa Afghanistan washuhudie utulivu.

Kufuatia mlipuko uliojiri jana Ijumaa katika msikiti wa Khan Abad karibu na mji wa Kunduz nchini Afghansitan, waumini wasiopungua 60 wameripotiwa kuuawa na wengine 150 kujeruhiwa. Baadhi ya duru zinasema waliouawa shahidi katika hujuma hiyo ni karibu 100.

Hujuma hiyo ya kigaidi ilijiri wakati waumini walipokuwa wakiswali Swala ya Ijumaa katika msikiti huo wa Waislamu wa madhehebu ya Shia. Hii ni hujuma ya kwanza kubwa kuwahi kutekelezwa dhidi ya Mashia wa Afghanistan tangu kundi la Taliban lichukue hatamu za uongozi mwezi Agosti. Kundi la kigaidi la ISIS limedai kuhusika na hujuma hiyo ambayo imelaaniwa vikali na viongozi wa Taliban.

4003428

captcha