IQNA

Al Azhar, Mufti Mkuu Misri walaani hujuma dhidi ya Msikiti wa Mashia Afghanistan

13:56 - October 09, 2021
Habari ID: 3474399
TEHRAN (IQNA)- Kituo cha Kiislamu cha Al Azhar Misri na Mufti Mkuu nchini humo wametoa taarifa na kulaani vikali hujuma ya kigaidi ya Ijumaa dhidi ya Msikiti wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia ambapo watu takribani 100 wameuawa.

Kwa mujibu wa tovuti ya Youm7, Al Azhar imelaani vikali hujuma iliyolenga msikiti huo katika mji wa Kunduz. Aidha Al Azhar imesisitiza kuwa inapinga vitendo vyote vya ugaidi na utumiaji mabavu katika maeneo ya ibada na kusisitiza kuwa vitendo kama hivyo ni kinyume cha mafundisho ya Uislamu na havina thamani na ubinadamu mbali na kuwa ni njama ya makusudi ya kuharibu taswira ya Uislamu.

Halikadhalika Al Azhar imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuungana katika kukabiliana na ugaidi. Kituo hicho cha Kiislamu Misri pia kimetuma salamu za rambi rambi kwa watu wa Afghanistan na familia za waathiriwa.

Katika taarifa nyingine, Mufti Mkuu wa Misri Sheikh Shawki Allam amelaani vikali hujuma hiyo ya kigaidi dhidi ya Msikiti wa Mashia mjini Kunduz. Ameongeza kuwa, Uislamu unapinga hujuma yoyote ile dhidi ya watu wasio na hatia na kuongeza kuwa jinai kama vile mauaji ni kati ya jinai mbaya zaidi na wahusika watapata adhabu kali duniani na kesho akhera.

Sheikh Allam amesema hujuma za kigaidi dhidi ya maeneo ya ibada ni ishara ya utambulisho wa kishetani wa wanaotekeleza uovu huo.

Kundi la kigaidi la ISIS au Daesh limedai kuhusika katika hujuma hiyo ya kigaidi ambayo ililenga waumini katika msikiti wa Mashia wakati wa Sala ya Ijumaa.

Makundi yanayofungamana na ISIS yana historia ndefu ya kutekeleza hujuma dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Afghanistan.

4003232

captcha