IQNA

Rais wa Zanzibar ataka jamii iwatunze walimu wa Qur’ani

20:34 - November 15, 2021
Habari ID: 3474562
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Zanzibar katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa wito kwa Waislamu kuwatunza na kuwaheshimu walimu wa shule za Qur’ani au Madrassah ili kuwapa motisha na kutambua jitihada zao za kuelimisha na kulea watoto.

“Kuna umuhimu wa jamii kuwatunza walimu wa Madrassah kwa kuandaa  mpango maalum wa kuwawezesha ili wahamasike katika ufundishaji , ikiwa pia ni hatua ya kuondokana na udhalili wa maisha walionao hivi sasa,” amesema Rais Mwinyi Jumapili wakati akifungua Madrasatul-Maryam iliyopo Zanzibar, Mfenesini Wilaya ya Magharibi “A ” Mkoa Mjini Magharibi.

 Aliwataka walimu na wazazi kuwahimiza watoto kudurusu masomo yao ili waweze kufanikiwa, huku akiunga mkono juhudi za Madrassah hiyo za kutoa msukumo katika ufundishaji wa muda wa ziada, hususan kwa wanafunzi wanaokabiliwa na mitihani ya Taifa ya mwisho wa mwaka.

 Alisema serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa madarassah ya kusomea katika skuli Unguja na Pemba, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na mrundikano wa wanafunzi uanosababisha kuwepo mikondo miwili ya masomo, hatua inayochangia wanafunzi kukosa muda wa kwenda madrasa kusoma masuala ya Dini.

 Aidha, aliutaka Uongozi wa Madrassah hiyo kuunda kamati kushughulikia uendeshaji wa Madrasa, ambapo pamoja na mamabo mengine itashughulikia suala la usafi.

 Rais Dkt. Mwinyi alisema mfadhili wa ujenzi huo tayari ametelekeza wajibu wake, hivyo akawataka waumini wengine kujitokeza kuendeleza ujenzi huo, akibainjisha wajibu huo kuwa ni wa watu wote na sio wa wafadhili pekee.

 Vile vile, alisiitiza umuhimu wa waumini kutoa sadaka kutoka miongoni mwa yale aliyowaruzuku Mwenyezi Mungu, kwa kigezo kuwa suala hilo limeelezwa katika Qur’ani Tukufu na hadithi za Mtume Muhammad (SAW) , huku akiwataka kutumia vyema majengo ya Ibada.

 Dk. Mwinyi aliwapongeza wahisani na watu wote waliotabaruki kwa njia mbali mbali na hatimae kufanikisha  ujenzi huo.

Aliahidi kuchangia upatikanaji wa kompyuta pamoja na kuahidi kushirikiana na wafadhili mbali mbali kufanikisha ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano wa madrassah hiyo.

Nae, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab alisema suala la ufunguzi wa madrasa sio kuwa ni la utamaduni wa Zanzibar, bali ni dini iliorithiwa kutoka Mtume Muhammad (SAW) pamoja na Masahaba zake.

Mapema, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume, akitoa salamu za Ofisi ya Mufti alisisitiza na kushajihisha usomaji wa Qur’ani, huku akifafanua kuwepo kheri , fadhila na ujira mkubwa kwa walimu wa Qur’ani, wanafunzi, waumini wanaosikiliza,  wazazi wa wanafunzi, wajenzi wa madrasa, pamoja na wale wanaofungua madrasa hizo.

Aliitaka jamii ya Wazanzibari kuwapa heshima wanayostahili walimu wa madrasa  ikiwa ni hatua ya kuondokana na udhalili uanowakabili hivi sasa.

PICHA : Rais Mwinyi akifungua Madrasatul-Maryam iliyopo Zanzibar, Mfenesini Wilaya ya Magharibi “A ” Mkoa Mjini Magharibi.

 

3476490

 

captcha