IQNA

Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Tanzania yamekuwa na mvuto mkubwa

19:58 - April 26, 2021
Habari ID: 3473851
TEHRAN (IQNA)- Mashindnao ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu yamefanyika Jumapili Aprili 25 katika uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam na kuvutia maelfu ya wakazi wa mji huo.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Djibrilla Hassane wa Nigeria, ameibuka mshindi wa kwanza na kujinyakulia Tz Sh 20milioni  katika mashindano ya 21  ya kuhifadhi kitabu cha Qur’an tukufu  kwa nchi za Afrika.

Mashindano hayo yaliandaliwa na Taasisi ya Al -Hikma Foundation chini ya udhamini wa Benki ya Watu wa Zanzibar  (PBZ ) 

Akitangaza washindi hao,  Jaji kiongozi wa mashindano hayo, Abdallah Almundhir, alisema mshindi wa pili alikuwa Hassan Hamad (Sudan) aliyepata Tz Sh 12 milioni. Huku akibainisha yalikuwa na ushindani  uliosababisha wakati mgumu majaji kuamua mshindi.

Alisema mshindi wa tatu ni Sangare Kalid wa Ivory Coast aliyepata Tz Sh 7.5 milioni,  wanne ni Omary Salim   wa Tanzania Tz Sh5 milioni na nafasi ya tano ilishikiliwa na Mustapha  Alliyu  wa Nigeria,  Tz Sh tatu milioni.  

Awali akizungumza  katika mashindano hayo, Rais wa Zanzibar wa  Dk. Hussein Mwinyi aliipongeza taasisi ya Al Hikma Foundation kwa kuendelea kuyaandaa mashindano hayo kwa mafanikio makubwa hasa  kwenye mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

“Natoa pongezi zangu kwa taasisi ya Al- Hikma Foundation  kwa jitihada kubwa wanayofanya kwa kuendelea kuandaa mashindano haya kwa ubora makubwa  kila mwaka bila kuchoka, nawapongeza kwa kuandaa mashindano haya ya 21 kwa mafanikio makubwa licha ya mwaka jana kuathirika na Covid-19, ” alisema.

Dk Mwinyi alieleza mwitikio mkubwa wa washiriki wakiwemo vijana kutoka ndani ya nchi kwenye mashindano hayo  ni kielelezo kizuri cha mafanikio.
Alitumia fursa hiyo kuwakaribisha washiriki wote kufurahia mazuri yote waliyoyaona wakiwa nchini na kuwa wawe mabalozi  kwenye mataifa yao.

“Inapendeza kuona Tanzania inaandaa mashindano yanayoshirikisha mataifa mengi na kwamba huo ni utamaduni mzuri ambao waasisi wa taifa letu walianza kuutengeneza,”alisema Dk  Mwinyi.

Alisema Tanzania bado inaendeleza utamaduni  kuishi kwa kupendana na kuwaomba washiriki wa mataifa mengine kuendelea kufurahia na kuwa mabalozi wazuri kwenye mataifa yao kwa kutangaza vivutio walivyoviona kupitia mashindano hayo.

Kwa uapnde wake, Wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaomba  Watanzania kuzidi kuliombea taifa  pamoja na viongozi wake ili Tanzania iwe kimbilio kwa watu wa mataifa mengine waliopoteza amani.

“Tuendelee kuliombea taifa na viongozi wake ili tuendelee kuwa na nchi kimbilio kwa wale wote waliopoteza amani kwao na atuepushe na mabaya yote ambayo yalitaka kutukabili,”alisema Majaliwa

Naye Mufti Mkuu wa Tanzania,  Sheikh Abubakar Zuberi  aliwapongeza wadau wote ikiwemo taasisi ya  Al Hikma Foundation kwa kuendelea kusimamia mashindano ya Afrika ya kuhifadhi Quran Tukufu.

Alisema mashindano hayo ambayo yanashirikisha mataifa mbalimbali ya Afrika ambayo yamefanyika miaka 20 yamesaidia kuitangaza Tanzania duniani.

“Ni mashindano makubwa tangu yameanza kufanyika ni mwaka wa 21 nawapongeza wadhamini wote hasa taasisi ya Al Hikma Foundation kwa kuendelea kusimamia na imesaidia kuitangaza nchi duniani,” alisema Sheikh  Zuber. 

3967336

captcha