IQNA

Tanzania mbioni kutunga sheria za benki za Kiislamu

14:18 - July 09, 2021
Habari ID: 3474084
TEHRAN (IQNA)- Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iko mbioni kutunga sheria za kuunga mkono mfumo wa Kiislamu wa benki nchini humo.

Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwigulu Nchemba amemtaka mwenyekiti wa taasisi ya Islamic Foundation Aref Nahdi ashirikiane na ofisi yake ili kutunga sheria hizo za benki za Kiislamu.

Nchemba ameyasema hayo alipokuwa akihutubu Alhamisi mjini Dar es Salaam katika  Mkutano wa Saba wa Mfumo wa Kiislamu wa Kifedha na Kibenki barani Afrika.  Akizungumza mapema katika kikao hicho Nahdi alilalamika kuwa ukosefu wa sheria umepelekea benki nchini humo kutotoa huduma za Kiislamu Tanzania na hivyo alitoa wito kwa Benki Kuu ya Tanzania kuzingatia utungaji sheria hizo.

Nchemba amesema benki ambazo tayari zinatoa huduma za Kiislamu kwa sasa zifuate viwango vilivyopo vya kimataifa.

Hivi karibuni Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) na Benki ya Dunia zilitangaza kanuni ambazo zinapaswa kufuatwa na benki za Kiislamu.

Benki ya Kenya Commercial Bank ya Kenya ilikuwa ya kwanza kuanzisha huduma za Kiislamu Tanzania mwaka 2008 na hivi sasa benki ya People’s Bank ya Zanzibar na Amana Bank nazo pia zinatoa huduma za Kiislamu.

Hafla hiyo imeandaliwa na AlHuda Centre of Islamic Banking and Economics (CIBE) na imedhaminiwa na Teknolojia ya ICD na Codebase, na inasaidiwa na SPM Consulting, CIFCA, na chuo cha London School of Modern Studies..

Washiriki wa ngazi za  juu kutoka nchi zaidi ya 20 wanatarajiwa kushiriki n.k. kutoka benki kuu, sekta za benki na fedha za Tanzania na nchi zingine za Kiafrika, na tasnia ya bima. 

3982808

captcha