Katika mahojiano na IQNA, Sheikh Ghazi Hanina, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maulamaa Waislamu Lebanon amesema katika nchi za Magharibi wale ambao kwa mfano kuna sheria za kupiga marufuku dhidi ya Mayahudi na wale wanaokiuka sheria hizo wanaadhibiwa. Ameongeza kuwa, "Hadi sasa hatujaona hatua zozote za kivitendo zikichukuliwa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) au Jumuiya ya Nchi za Kiarabu au mabaraza yoyote mengine katika nchi za Kiislamu kuzuia mauaji ya Waislamu."
Aidha amebainisha masikitiko yake kuwa baadhi ya mitandao ya kijamii imegeuka na kuwa vituo vya kueneza mifarakano na hitilafu baina ya Waislamu badala ya kueneza elimu na muongozo.
Halikadhalika amesema baadhi ya vituo vya televisheni vinatumika kuhimiza itikadi za ukufurushiaji na mifarakano baina ya Waislamu na kupelekea kuuawa Waislamu wasio na hatia katika nchi kama vile Afghanistan, Syria na Yemen.
Sheikh Hanina amesema moja ya nukta ambazo zinaweza kuleta nguvu katika Umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa, chanjo cha umoja ni imani kwa Allah SWT, Mtume Muhammad SAW na Qurani Tukufu.
Mwanazuoni huyo wa Kiislamu Lebanon amesema kati ya changamoto za kufikia umoja wa Waislamu ni hitilafu za kifiqhi. Amesema Katika zama za awali za Uislamu, hitilafu hizo za kina zilikuwa zikijadiliwa na wasomi katika vituo vya utafiti wa Kiislamu na hazikuwa mada za kujadiliwa kila mahala.