IQNA

Salamu za Rais wa Iran kwa mnasaba wa Maulid ya Mtume SAW

17:44 - October 24, 2021
Habari ID: 3474464
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Ebrahim Raisi ametuma salamu maalumu na mkono wa baraka na fanaka kwa viongozi wa nchi za Kiislamu kwa mnasaba wa maadhimisho ya kukumbuka kuzaliwa Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad Muhammad SAW na Wiki ya Umoja wa Kiislamu.

Katika jumbe hizo Sayyid Ebrahim Raisi amesema: Ni matarajio kwamba katika siku hizi adhimu na zenye baraka tele za Maulidi na sherehe ya kuzaliwa ruwaza njema, Muhammad SAW  tutafanya jitihada kubwa za kuimarisha mahusiano endelevu na imara kwa ajili ya kunyanyua juu zaidi Uislamu na kueneza sira na mienendo ya Mtume wa Rehma, Muhammad SAW kwa kutumia mafundisho ya dini hiyo yanayotukutanisha sisi sote pamoja na azmaa yetu ya udugu wa kiimani.

Leo tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiu Awwal 1443 Hijria inasadifiana na siku aliyozaliwa Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad bin Abdullah SAW na mjukuu wake mwema, Imam Ja'far al Swadiq AS.

Maulama na wanahistoria wengi wa Kiislamu wanasema kuwa, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Mwaka wa Tembo katika mji mtakatifu wa Makka. Baadhi ya wasomi hao wamesema alizaliwa tarehe 12 mwezi huo huo, na kwa msingi huo mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayati Imam Ruhullah Khomeini aliitangaza wiki moja ya kuanzia tarehe 12 hadi 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal kuwa Wiki ya Umoja baina ya Waislamu na siku za kusherehekea na kuadhimisha kuzaliwa kwa mtukufu huyo.

Kwa minasaba ya siku hii ya sherehe za Maulidi na kuzaliwa Mbora wa Viumbe Muhammad Mwaminifu SAW na mjukuu wake, Imam Swadiq AS, Shirika la Habari la IQNA Linatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu kote duniani.

132189

captcha