IQNA

Sheikh Shaltut, mbeba bendera ya umoja wa Kiislamu

10:34 - October 30, 2021
Habari ID: 3474491
TEHRAN (IQNA)- Sheikh Mahmoud Shaltut wa Misri alikuwa miongoni mwa wanazuoni walioanzisha harakati ya kukurubisha madhehebu za Kiislamu na alitoa fatwa ya kihistoria kuhusu Ushia.

Sheikh Mahmoud Shaltut alizaliwa tarehe 5 Shawwal mwaka 1310 (Aprili 23, 1893) katika kijiji cha Minyat Bani Mansur katika mkoa wa Buhayrah nchini Misri katika familia ya wanazuoni. Baba yake Sheikh Muhammad alimpa jina la Mahmoud na akafanya jitihada kubwa za kumlea na kumuelemisha mwanae.

Tangu hapo awali, kijana Mahmoud alionekana kuwa hodari na mwenye kipawa kikubwa katika kazi zake. Kwa sababu hiyo ami yake alimpeleka katika maktaba ya kijiji kwa ajili ya kupata elimu na maarifa ya Kiislamu. Miongoni mwa sheria na kanuni za maktaba za Misri za wakati huo ilikuwa ni mwanafunzi kuhifadhi moyoni Qur'ani nzima kabla ya kuanza kupata masomo ya fasihi ya lugha ya Kiarabu. Mahmoud, kama walivyokuwa wanafunzi wenzake, alilazimika kuhifadhi Qur'ani kabla ya jambo lolote na akafanikiwa kuhifadhi Qur'ani nzima katika kipindi kifupi.

Kipaji cha Sheikh Shaltut

Kipindi cha Kukamilisha Masomo Mwaka 1328 Hijria Kamaria (1906) Mahmoud alihamia katika mji wa Alexandria kwa ajili ya kupata elimu ya juu na akaanza masomo katika Chuo cha Alexandria. Uhodari wake wa kielimu na kipaji chake kikubwa kiliwashangaza walimu na wanafunzi wa chuo hicho. Baada ya kufanya bidii kubwa katika masomo, hatimaye mwaka 1340 (1918) alifanikiwa kupata shahada ya juu kabisa ya Chuo cha Alexandria na kuwa mwanafunzi bora wa chuo hicho akiwa na umri wa miaka 25. Mwaka mmoja baada ya kuhitimu masomo yaani mwaka 1341 Hijria (Februari 1919), Sheikh Shaltut alianza kufundisha katika chuo hicho.

Kuingia Al Azhar

Shaltut alijiunga na Chuo Kikuu cha al Azhar wakati wa Sheikh Muhammad Mustafa Maraghi ambaye alikuwa na taathira kubwa mno katika itikadi za Shaltut alipochaguliwa kuwa mkuu wa Chuo cha al Azhar mwaka 1360 Hijria (1938) na kusoma makala iliyokuwa imeandikwa na Sheikh Mahmoud Shaltut, alivutiwa mno na fikra za msomi huyo kijana, umahiri wake mkubwa wa fasihi ya lugha ya Kiarabu na uwezo wake mkubwa wa kutumia lugha hiyo katika maandishi.

Mwaka 1379 (1937 Miladia) Sheikh Shaltut aliteuliwa kuwa Kaimu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha al Azhar. Miaka minne baadaye yaani mwaka 1961, Rais wa wakati huo wa Misri alimteuwa Sheikh Mahmoud Shaltut kuwa mkuu wa chuo cha al Azhar.

Kufundisha Fiqhi ya Kishia

Miongoni mwa hatua muhimu za Sheikh Shaltut wakati wa uongozi wake katika chuo cha al Azhar ilikuwa ni kuanza kufundisha fiqhi ya madhehebu ya Shia Imamiyya sambamba na fiqhi ya madhehebu za Ahlusunna. Kazi nyingine muhimu ya Sheikh Shaltut ilikuwa ni kuanzisha shughuli za kukumbuka siku ya Shuraa na vikao vya kuomboleza kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein (as) katika chuo cha al Azhar. Suala hilo lilionesha mapenzi yake makubwa kwa Ahlyl Bait wa Mtume hususan Imam Hussein (as).

Fatwa ya kihistoria

Wakati alipokuwa Sheikh wa al Azhar, Sheikh Mahmoud Shaltut alipata fursa ya kutoa fatuwa yake ya kihistoria iliyojuzisha kwa wafuasi wa madhehebu za Kisuni kufuata madhehebu ya Kiislamu ya Shia J'afariya. Fatuwa (Fatwa) hiyo muhimu na ya aina yake ya Sheikh Shaltut ilitiwa saini na wanachama wa Darul Taqrib. Fatuwa hiyo wa Sheikh wa al Azhar ilikuwa na mwangwi mkubwa katika nchi za Kiislamu na kuzinawirisha fikra za watu safi na imani kubwa ya kidini za waliokuwa na azma kubwa ya kukurubisha pamoja Waislamu wa madhehebu zote.

Kutetea wanazuoni wa Iran

Siku sita baada ya tukio la mauaji ya tarehe 5 Juni 1963 na kutiwa mbaroni wanazuoni wa Kiislamu nchini Iran akiwemo Imam Khomeini, Sheikh Mahmoud Shaltut alitoa taarifa akiwataka Waislamu wote kuwaunga mkono wanazuoni wa Kiislamu waliotiwa nguvuni nchini Iran kwa kosa la kutetea haki. Katika taarifa hiyo Sheikh Shaltut alikemea mno kitendo cha kutiwa nguvuni wanazuoni hao wa Kiislamu na kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu akikitaja kuwa ni aibu kubwa kwa wanadamu. 

Sheikh Mahmoud Shaltut aliaga dunia tarehe 27 Rajab mwaka 1383 Hijria Qamariya na kuiacha jamii ya Kiislamu katika majonzi makubwa.

4008504

captcha