IQNA

Wale wasio na chanjo ya COVID-19 watakiwa kutohudhuria Sala ya Ijumaa Singapore

16:36 - January 29, 2022
Habari ID: 3474863
TEHRAN (IQNA)- Baraza la Kiislamu la Singapore (Muis) limewataka wale ambao bado hawajapata chanjo ya COVID-19 wajizuie kushiriki katika Sala ya Ijumaa kutokana na sababu za kiafya.

Jumamosi Baraza la Kiislamu Singapore limetoa taarifa kupitia Ofisi ya Mufti na kutoa ushauri wa kidini kuhusu sala za jamaa misikitni. Taarifa hiyo imeshauri kuwa wale wanaojihisi kuwa ni wagonjwa au hawajapata chanjo ya COVID-19 wanapaswa kujilinda na kuwalinda waumini wengine kwa kusali Sala ya adhuhuri nyumbani badala ya Sala ya Ijumaa msikitini. 

Baraza hilo limewashauri waumini, hasa wanaume, kuchukua hatua ziwezekanazo ili kuhakikisha kuwa wanashiriki katika Sala ya Ijumaa. Kati ya hatua hizo ni kupata chanjo ya COVID-19 na kujisajili mapema kushiriki katika Sala ya Ijumaa.

Taarifa ya Muis imesema ushauri huo utabadilika kadiri hali ya COVID-19 inavyozidi kubadilika nchini humo.

Singapore au Singapuri ni nchi ndogo na iliyostawi katika Asia ya Kusini-Mashariki ambayo uchumi wake unategemea zaidi biashara, hasa benki pamoja na viwanda. Waislamu wanakadiriwa kuwa asilimia 15 ya watu wote milioni 5.6 katika nchi hiyo.

Singapore ina sheria kali za kuzuia matamshi au maandishi ya chuki na vitendo vyote ambavyo vinaweza kuibua uhasama baina ya wafuasi wa dini mbali mbali nchini humo.

/3477584

captcha